Na Saulo Stephen - Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amesema Mkoa wa Singida umeanza kwa vitendo utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na umejipanga kuwa miongoni mwa mikoa itakayoongoza kitaifa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, utoaji wa huduma bora na ukuaji wa uchumi.
Dendego ameyasema hayo wakati akiongea kwenye na wananchi kwenye viwanja vya Maonesho Mandewa, amesema Mkoa unaendelea kuwa salama, wenye amani na chakula cha kutosha, huku wananchi wakiendelea kunufaika na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema Singida imeendelea kupokea rasilimali fedha, watumishi na vifaa vinavyowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kwamba miongoni mwa mafanikio hayo ni ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali na maboresho yanayoendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, hatua zinazoongeza upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi wa TACTIC wenye thamani ya shilingi bilioni 24.5 unaendelea, ukiwa unahusisha ujenzi wa soko la kisasa la vitunguu, barabara za lami zenye urefu wa kilometa 7.2 pamoja na mifereji ya maji ya mvua.
Pia Mahakama Kuu Tawi la Singida imeanza kutoa huduma, huku mradi wa Uwanja wa Ndege wa Singida ukiendelea ambapo wataalamu tayari wamewasili kwa ajili ya utekelezaji wake.
Aidha Dendego amewahimiza wananchi kutumia fursa zinazotokana na miradi hiyo kuongeza kipato na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya mkoa.
Amesisitiza kuwa Singida imejipanga kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kasi na ufanisi, akibainisha kuwa lengo la Mkoa ni kubaki miongoni mwa mikoa inayoongoza kitaifa katika utekelezaji wa mipango ya Serikali na utoaji wa matokeo yenye tija kwa wananchi.
Discussion
Reader comments
0 contributions