Teknolojia imeendelea kukua kwa kasi katika kipindi cha zaidi ya miaka 50, kiasi kwamba simu janja (smartphones) tunazotumia leo zina uwezo mkubwa zaidi wa kuchakata taarifa kuliko kompyuta iliyotumika kusaidia safari ya kihistoria ya Apollo 11 iliyowafikisha binadamu mwezini kwa mara ya kwanza mwaka 1969.
Kwa mujibu wa wataalamu wa teknolojia, baadhi ya simu za kisasa zina uwezo wa kufanya mamilioni ya hesabu kwa muda mfupi sana, kuhifadhi taarifa nyingi na kutekeleza programu mbalimbali kwa wakati mmoja, uwezo ambao ulikuwa nje ya mipaka ya kompyuta nyingi zilizokuwepo wakati wa safari hiyo.
Julai 20, 1969, shirika la anga za juu la Marekani (NASA) liliandika historia baada ya wanaanga Neil Armstrong na Buzz Aldrin kutua mwezini kupitia safari ya Apollo 11, huku Michael Collins akiendelea kuzunguka mwezi akiwa ndani ya chombo cha angani.
Mafanikio hayo yalisaidiwa na kompyuta maalumu iliyojulikana kama Apollo Guidance Computer (AGC), iliyotengenezwa kwa ushirikiano na wataalamu wa Massachusetts Institute of Technology (MIT).
Kompyuta hiyo ilikuwa na jukumu la kufanya hesabu za mwelekeo, kufuatilia nafasi ya chombo angani na kusaidia kudhibiti safari na kutua mwezini. Ingawa haikuwa kompyuta ya kwanza duniani, ilikuwa miongoni mwa mifumo ya kisasa zaidi ya kudhibiti vyombo vya angani katika kipindi hicho.

Tofauti kubwa kati ya kompyuta hiyo na simu za sasa inaonekana katika uwezo wa kumbukumbu na kuhifadhi taarifa.
Apollo Guidance Computer ilikuwa na kumbukumbu ya muda (RAM) ya takribani kilobaiti 4 pekee na kumbukumbu ya programu ya takribani kilobaiti 72.
Kwa kulinganisha, smartphone yenye RAM ya gigabaiti 8 ina kumbukumbu ya muda iliyo takribani mara milioni mbili zaidi ya kompyuta hiyo, huku simu zenye uwezo wa kuhifadhi gigabaiti 128 au 256 zikiwa na nafasi ya kutunza mamilioni ya mara zaidi ya taarifa.
Hii ina maana kuwa picha moja ya kawaida inayopigwa kwa simu ya kisasa inaweza kuwa na ukubwa unaozidi kwa mbali kumbukumbu yote ya programu iliyokuwa ndani ya kompyuta ya Apollo 11.
Sababu nyingine inayoifanya smartphone kuwa na uwezo mkubwa ni maendeleo ya processor, ambayo ni sehemu kuu inayofanya hesabu na kuchakata maelekezo.
Kompyuta ya Apollo ilikuwa na kasi ya saa ya takribani megahertz 1.024, wakati processor za simu nyingi za sasa zinafanya kazi kwa kasi ya gigahertz kadhaa na zina viini vingi vya uchakataji (CPU cores).
Teknolojia hiyo inaruhusu simu kuendesha programu kadhaa kwa pamoja, kuhariri video, kucheza michezo yenye picha za ubora wa juu na kufanya hesabu changamano ndani ya sekunde chache.
Aidha, simu za kisasa zina vitengo maalumu vya kuchakata picha (GPU) na akili bandia (NPU), vinavyosaidia kutambua picha, kutafsiri lugha, kuboresha kamera na kuendesha baadhi ya mifumo ya AI bila kutegemea intaneti.
Maendeleo ya teknolojia ya utengenezaji wa chip yamechangia kwa kiasi kikubwa tofauti hiyo. Wakati wa Apollo 11, kompyuta ilihitaji vipuri vingi vya kielektroniki na ilikuwa na uzito wa takribani kilogramu 32, huku ikitumia umeme wa karibu wati 70.
Leo, watengenezaji wa simu wameweka mabilioni ya transistor ndani ya chip ndogo yenye ukubwa wa sentimita chache tu.
Transistor hizo hufanya kazi ya kushughulikia ishara za kielektroniki na kutekeleza maelekezo kwa kasi kubwa, huku teknolojia ya kisasa ikisaidia kupunguza matumizi ya nishati. Ndiyo sababu smartphone inaweza kufanya kazi nyingi kwa kutumia betri ndogo inayoweza kuchajiwa na kubebwa mfukoni.
Smartphone pia ina uwezo mkubwa wa mawasiliano na ukusanyaji wa taarifa kuliko kompyuta iliyotumika kwenye Apollo 11.
Simu za sasa zina GPS kwa ajili ya kutambua mahali, kamera zenye uwezo mkubwa, vihisi mwendo, intaneti ya kasi kupitia 4G na 5G, pamoja na teknolojia za Wi-Fi na Bluetooth.
Kupitia uwezo huo, mtumiaji anaweza kuwasiliana na mtu aliyepo upande mwingine wa dunia, kuona ramani, kufanya miamala ya fedha, kuhudhuria mikutano ya video na kupata taarifa kwa wakati halisi.
Apollo Guidance Computer haikuwa na uwezo huo wa matumizi ya kila siku, kwa kuwa iliundwa mahsusi kutekeleza majukumu ya kuongoza na kudhibiti chombo cha angani.

Wataalamu wanaeleza kuwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuchakata taarifa hakumaanishi kwamba smartphone ya kawaida inaweza kutumika moja kwa moja kuongoza chombo cha angani hadi mwezini.
Kompyuta ya Apollo iliundwa kwa ajili ya kazi maalumu iliyohitaji usahihi, utegemezi mkubwa na uwezo wa kufanya maamuzi ya haraka katika mazingira hatarishi.
Programu zake ziliandaliwa kwa namna ambayo ingeweza kuyapa kipaumbele majukumu muhimu hata wakati kompyuta ilipokuwa imeelemewa na kazi.
Mfumo huo ulikuwa sehemu ya mtandao mpana wa vifaa vya urambazaji, rada, mawasiliano na wataalamu waliokuwa wakifuatilia safari kutoka duniani.
Tofauti kati ya Apollo Guidance Computer na simu za kisasa inaonesha ukubwa wa maendeleo ya teknolojia ya binadamu ndani ya miongo michache.
Kifaa ambacho leo kinatumika kupiga picha, kuwasiliana kwenye WhatsApp, kutazama video na kucheza michezo kina uwezo wa kuchakata taarifa unaozidi kwa mbali kompyuta iliyosaidia kufanikisha moja ya safari muhimu zaidi katika historia ya binadamu.
Mafanikio ya Apollo 11 yanaendelea kuwa ushahidi kwamba ubunifu, uhandisi na matumizi sahihi ya teknolojia vinaweza kufanikisha mambo makubwa, hata wakati vifaa vinavyopatikana vina uwezo mdogo ukilinganisha na teknolojia ya sasa
Discussion
Reader comments
0 contributions