Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) limeendelea kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini kupitia uwezeshaji wa wajasiriamali, akieleza kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu shirika hilo limefanikiwa kuanzisha viwanda 1,760 na kuzalisha zaidi ya ajira 60,000.
Amesema mafanikio hayo yanaonesha umuhimu wa kuwekeza katika wajasiriamali wa ndani ili kuongeza uzalishaji, kupanua fursa za ajira na kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa nchini, hatua inayoweza kuongeza kipato cha wananchi na kuimarisha uchumi wa Taifa.
Kapinga ameyasema hayo Oktoba 24, 2026, wakati akizindua rasmi Maonesho ya 5 ya SIDO Kitaifa katika Uwanja wa Magufuli, Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, yaliyowakutanisha wajasiriamali na wadau mbalimbali wa sekta za umma na binafsi.
“Tunapoangazia kujenga uchumi wa Taifa, tunaweka nguvu katika uwekezaji wa ndani ili kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi. Hilo ndilo mojawapo ya malengo ya kuanzishwa kwa SIDO,” amesema Kapinga.

Amesisitiza kuwa Serikali inatarajia kuona wajasiriamali wakitoka katika hatua ya kuuza mazao ghafi na kuelekea katika kuyachakata kwa kutumia teknolojia zinazofaa, ili kuongeza thamani ya bidhaa, kupanua masoko na kuongeza mapato yao.
Amesema uwekezaji katika teknolojia za uchakataji ni muhimu kwa kuwa utawasaidia wananchi kutumia rasilimali zinazopatikana katika maeneo yao kuzalisha bidhaa zenye thamani kubwa zaidi, badala ya kutegemea kuuza mazao bila kuyafanyia uchakataji.
Katika hatua nyingine, Waziri Kapinga amesema Serikali inatambua upatikanaji wa mitaji kuwa nguzo muhimu katika kukuza ujasiriamali na kuendeleza viwanda vidogo, hivyo inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa mikopo nafuu kupitia mifuko ya taifa inayolenga kuwawezesha wajasiriamali.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha huduma hizi zinawafikia wajasiriamali wengi zaidi, ili waweze kuanzisha na kuendeleza biashara zao, kuongeza uzalishaji na kutengeneza ajira,” amesisitiza.

Awali, akisoma taarifa ya shirika hilo, Kaimu Mkurugenzi wa SIDO Ahmed Kitara, amesema shirika hilo limetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 14 kwa wajasiriamali ambapo asilimia 52 ya mikopo hiyo imetolewa kwa wanawake.
“SIDO tumefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi Bilioni 12 kwa wajasiliamali ambpo asilimia 52 ya mikopo hiyo imetolewa kwa anawake na wapo hapa kwenye maonesho yam waka huu na wanaendelea kufanya vizuri” Amesema Kitara.
Kla ya uzinduzi huo, Kapinga ametembelea baadhi ya mabanda ya wajasiriamali na kujionea bidhaa mbalimbali zilizobuniwa na kutengenezwa na Watanzania kupitia viwanda vidogo vilivyopo nchini.
Maonesho hayo yanaendelea katika Viwanja vya Magufuli manispaa ya Kahama, yakitoa fursa kwa wananchi kutembelea mabanda, kununua bidhaa, kujifunza na kupata mafunzo kutoka kwa wataalamu wa sekta ya viwanda huku kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni “Teknolojia na masoko, Chachu ya Viwanda Vidogo Nchini."

Discussion
Reader comments
0 contributions