Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imeanzisha mfumo wa malipo ya kabla ya kutumia maji katika vituo vya kuchotea maji vya pamoja vinavyojulikana maarufu kama magati, hatua inayolenga kuboresha usimamizi wa huduma ya maji na kuongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato.

MKURUGENZI MTENDAJI WA MAMLAKA YA MAJI SAFI NA USAFI WA MAZINGIRA SHUWASA YUSUPH KATOPOLA
Akizungumza leo wakati wa zoezi la ukaguzi wa vituo hivyo katika kata za Mwamalili Old Shinyanga Kambarage Mjini na Ibadakuli mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Shinaynga (SHUWASA) mhandisi Yusuph Katopola amesema mfumo huo unatarajiwa kurahisisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi, kudhibiti changamoto za malimbikizo ya madeni pamoja na kuhakikisha kila mtumiaji analipia kiasi cha maji anachotumia.
Amesema , hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za SHUWASA katika kuboresha utoaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Manispaa ya Shinyanga na kuanisha kwamba wanatekeleza mmradi huo kwa kushirikiana na kampuni ya E WATER SERVICES kutoka nje ya nchi na kwamba mfumo huo wa malipo ya kabla unamuwezesha mwananchi kuchota maji kwa uhuru kwa hauhitaji muuza maji kuwa katika eneo la tukio.
Ameongeza kuwa mwananchi atapewa token ambayo ataweka kiasi cha fedha kuanzia shilingi 500 na kuendelea na wakati wowote atakapohitaji maji hana haja ya kumsubiria muuzaji bali atakuja katika gati na kuingiza tokeni kisha kuchota maji kwa namana anavyoitaji kutokana na kiasi cha fedha alichoweka.
Katopola ameongeza kuwa mfumo huo ni njia moja wapo ya kuiongezea makusanyo SHUWASA kwani ni mchakto wa kuchukua fedha kabla ya huduma na kupelekea mamlaka hiyo kutolimbukiza madeni kwani nyakati za nyuma wauzaji katika magati haya walikuwa wakiuza maji na kisha kupeleka fedha hizo katika mamlaka hiyo lakini baadhi yao hawakuwa waaminifu katika kufikisha fedha zote na kupelekea mamlaka kuwa na madeni makubwa.

MENEJA ANKARA NA MDHIBITI WA MADENI SHUWASA TWALIB ABBAS
Akitoa ufafanuzi kuhusiana na mfumo huo meneja ankara na mdhibiti wa madeni SHUWASA Twalib Abbas ameeleza kuwa wananchi wanaotegemea huduma za maji katika magati wote watapatiwa tokeni kisha kujaza fedha na kisha magati husika yatamuhudumia mteja kwa mfumo wa lita kwa namna mteja anavohitaji
Twalib amesema iwapo fedha itaisha katika kadi basi mwananchi hawezi kupata maji kwani viwango husika vimeshawekwa moja kwa moja kwa mujibu wa EWURA kulingana na kiasi ambacho kinakatwa kwa ujazo wa lita moja kwa maana ya ujazo wa ndoo ya lita 20
"Ndani ya gati hili kuna valve ukiweka hii kadi hapa maji yatafunguka yatatoka na mteja atachita maji "amesema Twalib

Nao baadhi ya wananchi akiwemo Spora Joseph mkazi wa kitongoji cha Ikulilo katika kijiji cha Uzogore ameipongeza SHUWASA kwa huduma hiyo kwai sasa wamekuwa wakipata maji muda wote tofauti na zamani muuzaji anpokuwa hayupo katika kituo walitembea umbali mrefu katika vijiji jirani kufata maji

MAKOYE NGUSA MFANYABIASHARA WA MAJI KATIKA KATA YA MJINI MANISPAA YA SHINYANGA
Lakini pia Makoye Ngusa mkazi wa kata ya mjini ambaye ni mfanyabiashara wa maji amesema huduma hiyo ya kulipa kabla na kupatiwa kadi imekuwa ni nzuri kwani bei imeshuka tofauti na zamani na kwamba kwasasa hata unapokuwa na shilingi 500 anachota maji na kwenda kuuza na kwamba amekuwa akijipatia kipato kinachomuendeshaea maisha yake
Kwa ujumla, utekelezaji wa mfumo wa malipo ya kabla katika vituo vya kuchotea maji vya pamoja maarufu kama magati unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuboresha usimamizi na utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi. Hata hivyo, mafanikio ya mradi huo yatategemea elimu itakayotolewa kwa watumiaji, upatikanaji wa huduma kwa urahisi pamoja na kuhakikisha mfumo huo unakuwa endelevu na wenye manufaa kwa jamii.

Discussion
Reader comments
0 contributions