Skip to main content

SHULE YA MSINGI KACHELI YA KASULU KUBADILISHWA MATUMIZI IWE SEKONDARI

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amesema Serikali inafanya mapitio ya kubadili matumizi ya Shule ya Msingi Kacheli iliyopo Kijiji cha Zeze, Wilaya ya Kasulu, kuwa Shule ya Sekondari.

SHULE YA MSINGI KACHELI YA KASULU KUBADILISHWA MATUMIZI IWE SEKONDARI
Studio Narration JAMBO FM

SHULE YA MSINGI KACHELI YA KASULU KUBADILISHWA MATUMIZI IWE...

0:00 --:--

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amesema Serikali inafanya mapitio ya kubadili matumizi ya Shule ya Msingi Kacheli iliyopo Kijiji cha Zeze, Wilaya ya Kasulu, kuwa Shule ya Sekondari.

Hatua hiyo inafuatia baadhi ya wakazi kutoka vitongoji visivyo rasmi vya Lugufu Relini na Kacheli, vilivyopo katika Hifadhi ya Misitu ya Mkuti, Wilaya ya Uvinza, kutowapeleka watoto wao katika shule hiyo licha ya kujengwa na Serikali kwa ajili yao.

Akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Zeze, Balozi Sirro amesema Serikali ya Mkoa imepokea maoni ya wananchi kuhusu umbali wa shule hiyo na imeamua kuanza utaratibu wa kuibadilisha kuwa Shule ya Sekondari.

Amesema mpango huo unalenga kuhakikisha shule hiyo inapokea wanafunzi wa Kidato cha Kwanza watakaohitimu elimu ya msingi mwaka 2027.

Kwa mujibu wa Balozi Sirro, uongozi wa Wilaya ya Kasulu ulikamilisha ujenzi wa Shule ya Msingi Kacheli mwaka 2024 na kutenga eneo kwa ajili ya makazi katika Kitongoji kipya cha Landani, Kata ya Rusesa, wilayani Kasulu.

Eneo hilo lilitengwa kwa ajili ya wananchi waliokuwa wamevamia Hifadhi ya Misitu ya Mkuti, ambao walitakiwa kuhamia katika eneo hilo. Hata hivyo, baadhi ya wananchi hao wameendelea kukaidi agizo hilo, huku wengine wakihamia maeneo mengine ndani ya Mkoa wa Kigoma.

Akifafanua kuhusu sababu za wakazi wa Kijiji cha Zeze kutowapeleka watoto wao katika Shule ya Msingi Kacheli, Balozi Sirro amesema Serikali imepokea malalamiko hayo na inaandaa utaratibu kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kubadili matumizi ya shule hiyo kutoka shule ya msingi kuwa ya sekondari.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wa Kijiji cha Zeze wamesema sababu kubwa ya kutowapeleka watoto wao katika shule hiyo ni umbali, ambao wanakadiria kuwa kati ya kilomita mbili hadi tatu kutoka kijijini hapo.

“Shule ya Msingi Kacheli imejengwa kwa ajili ya waliovamia hifadhi, hivyo hatuko tayari kupeleka watoto huko kwa sababu ni mbali na kijiji na tunahofia usalama wa watoto wetu wakiwa njiani,” amesema Salome Moshi, mkazi wa Kitongoji cha Nyakitanga, Kijiji cha Zeze.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.