Na Eunice Kanumba –Shinyanga.
Katika kuendeleza jitihada za kuboresha huduma za afya kwa wananchi leo tarehe 21 April 2026 imezinduliwa kliniki maalum ya Himofilia katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga MWAWAZA , ikiwa ni hatua muhimu ya kuokoa maisha ya wagonjwa wanaokabiliwa na changamoto ya kutokuganda kwa damu.
Kuganda huko ni hali ya kawaida inayotokana na upungufu wa vinasaba vinavyohusisha na kugandisha damu,(clotting factors) hatua inayotarajiwa kupunguza adha kwa wagonjwa wanoasumbuliwa na mardhi hayo kusafiri umbali mrefu kufuata huduma zakitabibu katika hospital ya kanda
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kiliniki hiyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Timothy Sosoma amesema tukio hilo ni la kihistoria na lenye umuhimu mkubwa katika juhudi za serikali kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi kwa usawa, bila kujali aina ya ugonjwa au mahali wanapoishi.

Amesema, Serikali kwa kushirikiana na wadau imendelea kuchua hatua katika kukabiliana na magonjwa mbalimbali yakiwemo ya damu na kwamba kuanzishwa kwa kiliniki hiyo ni matokeo ya mashirikiano kati ya wizara ya afya ,hospital ya taifa ya muhimbili pamoja na chama cha himofilia Tanzania kwa ufadhili wa mashirika ya Novo Nordiskh hemophilia, Haemoblobinopathies Foundation pamoja na Novo Nordisk Foundatio
Ameeleza kuwa kupitia mradi huo, wataalam wa afya wamepatiwa mafunzo ya kina kuhusu namna ya kuwahudumia wagonjwa wa himofilia, yakihusisha kada mbalimbali ikiwemo madaktari, wauguzi, wataalam wa maabara, wafamasia na wataalam wa tiba ya viungo na kwamba sasa wapo tayari kutoa huduma kwa wagonjwa himofilia watakofika katika hospitali hiyo kupata matibabu.
Sosoma amesema mafunzo hayo hayakuishia katika hospitali ya rufaa pekee, bali pia yamefika katika hospitali zote za wilaya ndani ya mkoa, hatua inayolenga kuhakikisha huduma bora zinapatikana kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu, pamoja na kutoa mafunzo hayo kwa watalamu wa tiba za asili ili katika kutimiza majukumu yao wanapokutana na mgonjwa mwenye dalili za himofilia wamuelekeze kufika hospitalini hapo kwani walio wengi uhusianisha ugonjwa huo na imani za kishirikiana kwa kuamini kuwa wamerogwa.

Amesema upatikanaji wa dawa za himofilia zinazotolewa bure kupitia Shirika la Himofilia Duniani (WFH), ni mafanikio makubwa kwa taifa, akibainisha kuwa dawa hizo ni ghali sana na ni muhimu katika kuokoa maisha ya wagonjwa na kuzuia madhara makubwa yanayoweza kusababishwa na ugonjwa huo.
Aidha, ametoa maelekezo kwa uongozi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga kuhudumia wagonjwa kwa weledi ikiwemo kuwa na mfumo madhubuti wa ufatiliaji wa dawa ili wagonjwa waweze kuhudumiwa kwa ufasaha pamoja na kuendelea kununua vitendanishi vya maabara ili kughakikisha vipimo vyote muhimu vinapatikana kwa wakati.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma za magonjwa ya damu na Katibu wa Chama cha Himofilia Tanzania, Dkt. Abdallah Makalla amesema uzinduzi wa kliniki hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kitaifa wa kuboresha huduma za himofilia nchini na kwamba ugonjwa wa himofilia unahitaji uelewa wa pamoja katika jamii kwani husababisha damu kushindwa kuganda kwa utaratibu wa kawaida hivyo kuhataraisha maisha ya mgonjwa
Akizungumizia kuimarishwa kwa kiliniki hiyo katika hospital ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga Makalla Amebainisha kuwa hospitali hiyo imepokea vitendanishi vya maabara vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 1.5, vifaa vya mazoezi ya viungo (physiotherapy) vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 3.5, pamoja na vifaa vingine muhimu.

“Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na friji maalum kwa ajili ya kuhifadhia dawa za wagonjwa wa Himofilia, friji kwa ajili ya huduma za fiziotherapia, kompyuta kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za wagonjwa, pamoja na vitendea kazi vingine vya zaidi ya shilingi milioni saba,” amesema Dr Makalla.
Aidha, ameongeza kuwa mradi huo pia umewezesha upatikanaji wa dawa za Himofilia zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 525 kwa ajili ya kusaidia wagonjwa, hatua inayotarajiwa kuboresha huduma na kupunguza hatari kwa wagonjwa hao.

Hata hivyo, ameeleza kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto ya upatikanaji wa taarifa sahihi za wagonjwa, hali inayoweza kuchelewesha upatikanaji wa dawa kutoka kwa wafadhili, hivyo kusisitiza umuhimu wa kuboresha mifumo ya ukusanyaji na utunzaji wa takwimu.
Naye, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Augustino Maufi amesema hospitali hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha wagonjwa wa himofilia wanapata huduma bora na za haraka, ili kuepuka vifo na ulemavu unaoweza kusababishwa na ugonjwa huo na kwamba wamejiandaa vizuri katika kuendesha kiliniki hiyo kwa kuwahudumia wagonjwa kwa weledi mkubwa.

Himofilia ni ugonjwa wa kurithi wa damu unaosababisha mwili kushindwa kugandisha damu kwa kawaida kutokana na upungufu wa vinasaba vya kugandisha damu (clotting factors). Hali hii hupelekea damu kuvuja kwa muda mrefu kuliko kawaida au kutokwa damu ndani ya mwilini,Hata hivyo, takribani asilimia 30 ya wagonjwa hupata himofilia bila kurithi (sporadic hemophilia), hali inayotokana na mabadiliko ya vinasaba (gene mutation) yanayotokea bila historia ya ugonjwa katika familia.

Dalili za himofilia ni pamoja na kutokwa na damu ndani ya mwili bila jeraha la wazi, hasa kwenye ubongo, misuli au maungio, pamoja na kuvimba na maumivu kwenye viungo kutokana na damu kuvuja ndani. Vilevile, mgonjwa anaweza kupata kutokwa na damu kwa muda mrefu isivyo kawaida baada ya kupata jeraha, pamoja na kutokwa na damu nyingi baada ya kufanyiwa upasuaji , kung’olewa jino au pindi mgonjwa anapofanyiwa tohara.
Discussion
Reader comments
0 contributions