Wafanyakazi 72 Wauawa Kwa Shambulio la Anga Mgodi wa Dhahabu Mpaka wa Sudan na Misri.
Kamati ya wanasheria wa haki za binadamu nchini Sudan imethibitisha kuwa takriban wafanyakazi 72 wamepoteza maisha kufuatia mashambulizi ya anga yaliyolenga mgodi wa dhahabu katika eneo la mpakani lenye mgogoro kati ya Sudan na Misri.
shambulio hilo la anga lilipiga mgodi uliopo kwenye mpaka unaogombaniwa na Serikali za Sudan na Misri.Taarifa hizo rasmi zimetolewa na jopo la watetezi wa haki za binadamu nchini Sudan, huku walionusurika wakieleza matukio ya sintofahamu na hofu kubwa katika eneo hilo la milimani.

Kikundi cha wanasheria kinachoongozwa na Emergency Lawyers, ambacho kinachunguza na kuweka kumbukumbu za ukatili katika vita vya Sudan, kimeituhumu Jeshi la Anga la Misri kuhusika na shambulio hilo.
Kwa mujibu wa duru kutoka Sudan Shambulio hilo ni la pili kutokea mwaka huu katika eneo la Jabal al-Uqaydat, baada ya shambulio jingine la anga linalodaiwa pia kufanywa na Misri likiua wafanyakazi 23 katika eneo hilo la uchimbaji mdogo wa dhahabu mwezi Juni.
Kufuatia hilo jeshi la Misri halikukiri mara moja kufanya mashambulizi ya sasa, wakati wa tukio la mwezi Juni lilieleza kuwa lilifanya "operesheni kubwa" dhidi ya uchimbaji haramu wa dhahabu ndani ya mipaka yake.

Mpaka kati ya Sudan na Misri umekuwa na mgogoro wa muda mrefu, huku nchi zote mbili zikidai kumiliki eneo la Halayeb Triangle lenye utajiri mkubwa wa maliasili. Hata hivyo, Cairo inasalia kuwa mshirika mkuu wa jeshi la serikali ya Sudan, linalopambana na kundi la mgambo la Rapid Support Forces (RSF).
"Shambulio la Jumamosi limesababisha vifo vya wachimbaji raia 72 kulingana na taarifa za awali, huku juhudi za kudhibitisha na kuhesabu idadi kamili ya waathirika zikiendelea," ilieleza taarifa ya Emergency Lawyers.
ndege ya vita ilitokea juu yao majira ya saa 2:00 asubuhi (0600 GMT) siku ya Jumamosi na kufanya mashambulizi mara tano.

Walionusurika walisema waliona miili ya watu waliokufa ikiwa imetapakaa chini wakati wakikimbia, huku ikihofiwa kuwa wengi zaidi wamenasa chini ya vifusi mbali sana na miji au vituo vya huduma za dharura.
Tangu mwezi Aprili 2023, vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 200,000 na kutengeneza janga kubwa la kibinadamu. Hali hii imewasukuma raia wengi kufanya kazi hatari za uchimbaji wa dhahabu ili kujikimu, huku sekta hiyo ikitumika pia kufadhili pande zote mbili zinazopigana.
Discussion
Reader comments
0 contributions