Na Gideon Gregory - Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa ametolea ufafanuzi ulipo kuhusu ongezeko la deni la taifa ambapo amesema Serikali inakopa fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye maeneo ya kujenga uchumi na kuimarisha ustawi wa Jamii.
Msigwa ameyasema hayo leo Juni 28,2026 Jijini Dodoma wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi na kukiri kuwa "Ni kweli kwamba Deni la Taifa limeongezeka".

"Serikali haikopi pesa ili kugawana kama njugu, Serikali inatumia mikopo kama nyenzo muhimu ya kugharamia utekelezaji wa bajeti na miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali za kimkakati,"amesema.
Amesema hadi kufikia mwezi Machi 2026, deni la Serikali lilifikia jumla ya shilingi trilioni 114.34. Kati ya kiasi hicho Shilingi trilioni 75.89 ni deni la nje, sawa na asilimia 66.37 ya deni lote, Shilingi trilioni 38.44 ni deni la ndani, sawa na asilimia 33.63 ya deni lote ambapo sehemu kubwa ya deni imekopwa nje.

"Tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Novemba, 2025 imeonesha kuwa viashiria vya deni la Serikali viko ndani ya wigo unaokubalika kimataifa katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu,"amesema.
Kadhalika Msigwa ameongeza kuwa tathmini hiyo inaonesha kuwa, thamani ya sasa ya deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 40.7 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55; thamani ya sasa ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 24.9 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40 na thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 125.4 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 180.

Ameeleza kuwa Tanzania inakopa kwa sababu inakopesheka, hivyo ingekuwa haikopesheki isingepewa fedha hizo.
"Wanaobeza kukopa waulizeni nchi gani ambayo haikopi? Waulizeni sisi uwiano wetu wa deni la Taifa kwa Pato la Taifa ni asilimia 40.7 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55, waulizeni nchi zilizoendelea Deni lao la Serikali limefikia asilimia ngapi? Zipo nchi kubwa tena kati 5 zenye uchumi mkubwa Duniani zimefikia asilimia 230, zipo zingine 170 nakadhalika. TUPO vizuri",ameeleza.
Discussion
Reader comments
0 contributions