Waziri wa Habari na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi za wananchi na mifumo ya usalama wa mtandao ili kukabiliana na ongezeko la uhalifu na utapeli unaofanyika kupitia teknolojia ya kidijitali.
Akizungumza Bungeni jijini Dodoma leo Alhamisi Novemba 05, 2026 wakati akiwasilisha Mkataba wa Umoja wa Afrika kuhusu Usalama wa Mtandao na Ulinzi wa Taarifa Binafsi wa mwaka 2014, maarufu kama Mkataba wa Malabo, kwa ajili ya kuridhiwa, Waziri Kairuki amesema, ongezeko la matumizi ya mtandao linaambatana na kuongezeka kwa matishio ya usalama na makosa yanayofanyika katika mazingira ya kidijitali.

Ameongeza kwa kusema kuwa, mkataba huo unalenga kuimarisha ushirikiano baina ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika katika kukabiliana na uhalifu wa mtandao, ambao unaweza kufanyika katika nchi moja na kuathiri watu au mifumo ya nchi nyingine bila kuzuiwa na mipaka ya kijiografia.
“Usalama wa mtandao ni jambo muhimu sana katika ustawi wa taifa lolote duniani, na kwa kadri matumizi ya mtandao yanavyoongezeka, ndivyo ambavyo matishio ya usalama wa mtandao na makosa yanayofanyika kupitia mtandao yanavyozidi kuongezeka,” alisema Kairuki.
Discussion
Reader comments
0 contributions