Na Gideon Gregory - Dodoma.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema, Serikali imeendelea kuweka mkazo kwenye motisha na fursa za elimu kwa watahiniwa wa kidato cha sita na vyuo vya ualimu, huku akisisitiza kuwa mafanikio yao yatafungua milango ya ufadhili wa masomo ndani na nje ya nchi.
Prof. Mkenda ameyasema hayo Mei 4,2026 Jijini Dodoma wakati akiwapokea walimu wapatao 150 wa amali waliokwenda kwenye ziara ya mafunzo ya mwezi mmoja nchini India, ambayo yatawawezesha kutoa elimu ya ufundi na mafunzo ya stadi za kazi nchini ili kukuza uchumi wa viwanda, kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana, na kuwajengea uwezo wa kushindana katika soko la ajira.

Aidha, Prod. ametumia wasaa huo kuwatakia kila mtuhani mwema wanafunzi wa kidato cha sita pamoja walimu ambapo amesema jumla ya wanafunzi 133,655 wameanza mitihani yao, huku walimu 14,679 nao wakiwa wameanza mitihani yao ya kuhitimu mafunzo rasmi ya ualimu.
Amesema hadi sasa mwenendo wa mitihani hiyo umekuwa mzuri na wa utulivu, huku serikali ikiwa imeendelea kuimarisha usimamizi ili kuhakikisha haki na uwazi vinatawala katika mchakato mzima wa upimaji.

“Hatupendi kupoteza mtu yeyote katika mitihani hii, lakini yeyote atakayekiuka kanuni tutamchukulia hatua,” amesema Waziri Mkenda, akionya dhidi ya udanganyifu.
Katika kuhamasisha ufaulu bora, amesema serikali imeendelea kutoa fursa mbalimbali kwa wanafunzi wanaofanya vizuri, ikiwemo kujiunga na vyuo vikuu na kupata mikopo kulingana na ufaulu wao pamoja na hali za kifamilia.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe ameshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 3 na kutoa kibali cha walimu hao kwenda kwenye ziara ya mafunzo nchini India ili kujifunza na kupata ujuzi utakaowawezesha kuleta athari chanya zaidi katika mfumo wa elimu ya ufundi.
Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amewataka walimu hao kuhakikisha yote waliyojifunza nchini India wanaenda kuwafundisha wanafunzi madarasani na kwa vitendo ili wapate ujuzi utakaowawezesha kuwa wabunifu, wajasiriamali na uwezo wa kushindana katika ajira za ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kujiajiri.

“Vijana wetu wanahitaji kupata maarifa na ujuzi mlioupata kwenye ziara yenu ya mafunzo nchini India, hivyo nendeni mkawafundishe kwa umahiri ili waje kutoa mchango katika maendeleo ya taifa,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Katika hatua nyingine, walimu walionufaika na mafunzo ya nje ya nchi wameeleza uzoefu wao, akiwemo Jackline Juliasi aliyepata mafunzo nchini India katika Chuo Kikuu cha Sharda, akisema wamejifunza matumizi ya teknolojia za kisasa za ufundishaji na tathmini za kidigitali.

Naye, Mwalimu Sungura Durunga amesema mafunzo hayo yamewafungua zaidi kuhusu umuhimu wa kuoanisha elimu na mahitaji halisi ya dunia, akisisitiza haja ya kuimarisha masomo ya teknolojia kama akili unde ili kuwajenga vijana wanaokwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Discussion
Reader comments
0 contributions