Shirika la World Vision Tanzania, limeikabidhi Serikali Mradi wa Maendeleo wa Buhoma uliotekelezwa katika tarafa ya Makere, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma, baada ya kukamilika kwa kipindi cha miaka 16 ya utekelezaji wake.
Mradi huo ulianza mwaka 2010 ukiwa na lengo la kuboresha maisha ya wananchi kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali za maendeleo, zikiwemo afya, elimu na maji na unatarajiwa kuhitimishwa rasmi Septemba 2026 baada ya kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii katika maeneo ya tarafa ya Makere.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mradi huo kwa Serikali, mwakilishi wa Meneja wa World Vision Tanzania, Steven Nyagonde, amesema mafanikio yaliyopatikana yanapaswa kulindwa kwa kuhakikisha kunakuwa na usimamizi mzuri wa miundombinu na miradi yote iliyoanzishwa kwa manufaa ya wananchi.
“Usimamizi mzuri wa miradi hii ndio nguzo muhimu ya kuendelea kutoa huduma kwa wananchi na jamii kwani tumeiacha katika katika hali nzuri na wananchi wameweza kunfaika nayo kwa kipindi chote hicho” alisema Steven Nyagonde.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, alisema Serikali itaendelea kusimamia na kutunza miradi yote iliyotekelezwa kupitia Mradi wa Buhoma kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya wananchi.
“Kumekuwa na ongezeko la kiwango cha ufaulu wa wanafunzi nah ii ni miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika miradi hii na tunaamini itaendelea kuwanufaisha wananchi lakini pia waendelee kuilinda ili iweze kudumu kwa muda mrefu” alisema Isaac Mwakisu.

Naye Mratibu wa Mradi wa Maendeleo wa Buhoma kutoka World Vision Tanzania Wilaya ya Kasulu, Esther Mushendwa, alieleza kuwa katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi huo, miundombinu mbalimbali ya huduma za kijamii imejengwa na kuboreshwa, hatua iliyochangia kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi wa Tarafa ya Makere.
Baadhi ya wananchi wa Tarafa ya Makere walieleza kuwa mradi huo umeleta mabadiliko makubwa katika maisha yao, hususan kwa kuboresha huduma za maji, afya na elimu, huku wakiiomba Serikali kuendelea kusimamia na kuendeleza miradi hiyo ili manufaa yake yaendelee kudumu kwa vizazi vijavyo.

Discussion
Reader comments
0 contributions