Skip to main content

SERIKALI YAKABIDHI ENEO LA UJENZI JENGO LA MAMA NA MTOTO, MAABARA YA KISASA SHINYANGA

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

SERIKALI YAKABIDHI ENEO LA UJENZI JENGO LA MAMA NA MTOTO, MAABARA YA KISASA SHINYANGA

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

Serikali kupitia Kampuni ya Ushauri Elekezi ya Volumetric Arch Consultant Ltd imekabidhi rasmi eneo la ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto la ghorofa tano pamoja na Jengo la Maabara ya Kisasa la ghorofa mbili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, hatua inayofungua rasmi utekelezaji wa mradi mkubwa wa kuboresha huduma za afya mkoani humo.

Makabidhiano hayo yaliyoambatana na utoaji wa Hati ya Makabidhiano ya Eneo la Ujenzi (Site Possession Certificate) yamefanyika leo Ijumaa Juni 5, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, yakihusisha wadau mbalimbali wa sekta ya afya, wataalamu wa ujenzi pamoja na mkandarasi anayetekeleza mradi huo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mshauri Mwelekezi wa Kampuni ya Volumetric Arch Consultant Ltd, Berno Batinamani, amesema mradi huo unatarajiwa kuanza rasmi Juni 19, 2026 na kukamilika mwaka 2028, ukiwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 22.

Amesema majengo hayo yatakapokamilika yataongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma za kisasa za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na maeneo ya jirani.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Tiba kutoka Wizara ya Afya ambaye pia ni Meneja wa Mkataba wa mradi huo, Festo Mapunda, amemtaka mkandarasi kuhakikisha kazi inatekelezwa kwa ubora unaotakiwa, kwa wakati uliopangwa na kwa gharama zilizokubaliwa kwenye mkataba.

Mapunda pia amesisitiza umuhimu wa kutumia nguvu kazi kutoka kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga ili kuwawezesha kunufaika na fursa za ajira zitakazotokana na utekelezaji wa mradi huo.

“Tunatarajia kuona mradi huu unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika. Aidha, wananchi wa Shinyanga wanapaswa kupewa kipaumbele katika ajira za muda zitakazopatikana wakati wa ujenzi,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya AMAR Builders Ltd, Mkandarasi anayejenga majengo hayo, Vipul Maran, amesema kampuni yake imejipanga kikamilifu kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vyote vya kitaalamu vinavyohitajika.

Amesema maandalizi ya awali ya utekelezaji wa mradi yamekamilika na kwamba wataendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali pamoja na mshauri mwelekezi ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa mafanikio.

Akizungumza kwa niaba ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. John Luzila, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya kupitia miradi mikubwa ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma za matibabu nchini.

Dkt. Luzila amesema, Jengo la Mama na Mtoto litakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 162 kwa wakati mmoja, hatua itakayosaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa na kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto katika mkoa huo.

Aidha, amesema jengo jipya la maabara ya kisasa lenye ghorofa mbili litaboresha huduma za uchunguzi na vipimo mbalimbali vya kitabibu, hivyo kuwawezesha wananchi kupata huduma nyingi za vipimo katika eneo moja bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.

Ameongeza kuwa, mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu ya afya nchini kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma bora za kisasa na zinazokidhi mahitaji ya wananchi, sambamba na kuendelea kuboresha huduma katika hospital za rufaa za mikoa.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.