Na Faustine Kasala - Kigoma.
Serikali imeendelea kuwekeza katika maendeleo ya usafiri majini Mkoani Kigoma kupitia maboresho ya Bandari ya Ziwa Tanganyika, ukarabati wa MV Liemba, ujenzi wa Meli mpya pamoja na kuimarisha huduma za utafutaji na uokoaji katika ziwa hilo.
Akizungumza na wanahabari kuelekea uzinduzi wa maadhimisho ya 16 ya siku ya Mabaharia Duniani ambayo Kitaifa yanatarajiwa kufanyika Mkoani Kigoma Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, IGP Mstaafu, Balozi Simon Sirro amesema, hatua hiyo imeongeza fursa za kibiashara uwekezaji utalii na ajira katika ukanda wa magharibi mwa Tanzania.

"Kwa kutambua mchango huu Mkubwa wa Serikali, niwaombe wananchia wote na wadau wa sekta ya usafiri wa majini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya 16 Siku ya Mabaharia Duniani Kitaifa hapa Mkoani Kigoma na kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha usalama wa usafiri majini na ustawi wa Mabaharia," amesema Balozi Sirro.
Kwa Upande wake Kaimu Meneja Mafunzo na utoaji vyeti kwa Mabaharia kutoka Shirika la Uwakala wa Meri Tanzania TASAC Eng Lameck Sondo amesema siku ya mabaharia ilianza rasmi kuazimishwa mwaka 2011 ikiwa na lengo la kutambua mchango wa mabaharia katika sekta nzima ya usafiri na usafirishaji.

"Mabaharia wana mchango mkubwa katika uchumi endelevu wa Dunia, ikubukwe kuwa Asilimia 90 ya Mizigo yote inayosafirishwa Duniani inasafirishwa kwa njia ya Majini hivyo Mabaharia wengi hupotezana na Familia zao na wengine hupoteza maisha kutokana na mazingira magumu ya kazi hii."
Aidha Eng Lameck amesema Shughuli zitakazo fanyika wakati wa Maadhimisho hayo ni pamoja na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu usalama wa usafiri majini, maonyesho ya huduma za Taasisi mbalimbali,Kampeni za matumizi salama ya vyombo vya usafiri majini na maonyesho ya uokoaji wakati wa dharura
Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi Tarehe 22 June 2026 katika viwanja vya Mwanga Community Center Mkoani Kigoma ambapo Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi-SMZ Dkt Khalid Mohamed anatarajiwa kuwa mgeni rasmi
Kwa Mwaka huu 2026 Maadhimisho hayo yamebebwa na Kauli mbiu isemayo "Kutoka Sera hadi utekelezaji kuimarisha ubora katika sekta ya usafiri majini"
Discussion
Reader comments
0 contributions