Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Prof. Tumaini Nagu, akimwakilisha Waziri wa Nchi, OWM–TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, ameitaka Mikoa na Halmashauri kutenga bajeti na kuimarisha huduma za lishe, afya, ulinzi na ujifunzaji wa awali ili kila mtoto apate nafasi ya kukua na kufikia uwezo wake.
Prof. Nagu ametoa maelekezo hayo Septemba 25, 2026, katika ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma, wakati akifunga Mkutano wa Tathmini ya Utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, kwa niaba ya Prof. Shemdoe.

Akieleza umuhimu wa hatua hizo, Prof. Nagu amesema Tanzania ina takriban watoto milioni 16, sawa na asilimia 27 ya wananchi kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2022. Amesema utafiti wa TDHS-MIS wa mwaka 2022 unaonesha kuwa asilimia 53 ya watoto wenye umri wa miaka miwili hadi minne wako katika hatari ya kutofikia ukuaji wao timilifu.
“Kutokana na matokeo hayo hatuna budi kuweka na kutekeleza mikakati thabiti ya kuimarisha huduma bora za malezi kwa watoto kuanzia ngazi ya familia, jamii na katika taasisi mbalimbali,” amesema Prof. Nagu.
Pamoja na changamoto hiyo, Prof. Nagu amesema utekelezaji wa programu umeleta maendeleo katika upatikanaji wa huduma. Idadi ya vituo vilivyosajiliwa vya kulelea watoto wadogo mchana imeongezeka kutoka 2,378 mwaka 2024 hadi 5,963 mwaka 2026, huku wamiliki na walezi 13,190 wa vituo hivyo wakipatiwa mafunzo tangu Januari 2022.

Amesema watoto 6,747,385 wamefikiwa na huduma ya chakula shuleni. Aidha, kufikia Juni 2026, vijiji na mitaa 17,560 kati ya 17,694, sawa na asilimia 99.2, vilikuwa vimetekeleza Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji. Kupitia siku hiyo, familia hupata fursa ya kufuatilia ukuaji wa watoto na kujifunza namna ya kuwaandalia vyakula vyenye lishe kwa kutumia vyakula vinavyopatikana katika maeneo yao.
Prof. Nagu amefafanua kuwa Serikali na wadau wamejenga jumla ya madarasa 1,316 ya elimu ya awali katika miaka ya fedha 2022/23 na 2023/24.
Ili kuendeleza mafanikio hayo, Prof. Nagu ameitaka Mikoa na Halmashauri kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya huduma za malezi na makuzi, kuhakikisha watoto wenye ulemavu na mahitaji maalumu wanajumuishwa katika mipango na bajeti, na kuwapatia walezi pamoja na wataalamu mafunzo ya kuwatambua watoto wanaohitaji huduma maalumu.
Pia ameitaka Mikoa kuhakikisha watoto walio katika vituo vya kulelea watoto wadogo mchana wanasajiliwa kwenye mfumo wa taarifa za shule.
Prof. Nagu ameisisitiza Mikoa na Halmashauri kujiandaa mapema kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua nyingi na mafuriko, hususan kwa kuhakikisha huduma za afya, maji salama, lishe na ulinzi wa watoto zinaendelea kupatikana.
Mkutano huo uliandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na OWM–TAMISEMI, Shirika la Children in Crossfire (CiC) na Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (TECDEN).
Discussion
Reader comments
0 contributions