Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka taasisi za umma kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini katika ujenzi, ununuzi wa samani na mahitaji mengine, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kukuza viwanda, kulinda ajira na kuongeza mapato ya Taifa.
Ametoa maelekezo hayo leo (Jumatano, Novemba 4, 2026), wakati akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 na Sera ya Maendeleo ya Jasiriamali Ndogo na za Kati ya Mwaka 2003 (Toleo la Mwaka 2025), katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma.
“Na jambo hili lianzie serikalini. Hata serikalini tunajenga majengo, tutumie bidhaa zinazozalishwa hapa nchini,” amesema.

Dkt. Mwigulu ametaja vioo, nondo, marumaru na samani kuwa miongoni mwa bidhaa zinazozalishwa nchini ambazo taasisi za umma zinapaswa kutumia, akisisitiza kuwa Serikali lazima iongoze kwa vitendo katika kutekeleza sera inazozitunga.
“Tumeweka sera, kwa hiyo lazima tuyaishi maneno yetu,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu ametaka sheria ziangaliwe na kurekebishwa iwapo zina mianya inayokwamisha matumizi ya bidhaa za ndani au kutoa nafasi ya kukwepa utekelezaji wa maelekezo hayo.
Amesema jitihada za kujenga viwanda haziwezi kuleta matokeo yaliyokusudiwa ikiwa bidhaa zinazozalishwa hazitumiki, kwa kuwa kukosekana kwa soko kunapunguza uzalishaji, ajira na mapato.

“Tutumie bidhaa zinazozalishwa nchini kwa kujiamini, kufurahia na kujivunia, ili kulinda viwanda vyetu, ajira na mapato ya nchi yetu, pamoja na kukuza uchumi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amewataka watendaji wa Serikali kubadili mtazamo kuhusu sekta binafsi na kuitambua kuwa mshirika muhimu katika kujenga uchumi unaojitegemea.
Amesisitiza umuhimu wa kuheshimu mitaji na uwekezaji, pamoja na kuendeleza mazingira yanayoiwezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.
Discussion
Reader comments
0 contributions