Na Adam Msafiri - Mara.
Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, imekusanya asilimia 86 ya lengo la mapato ya ndani katika mwaka wa fedha uliopita, huku kushuka kwa bei ya mazao ya biashara ya pamba na tumbaku kukitajwa kuwa miongoni mwa sababu zilizochangia kupungua kwa makusanyo hayo.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ayub Makuruma, amesema uchumi wa wilaya unategemea kwa kiasi kikubwa mazao hayo, hivyo kushuka kwa bei yake kumeathiri uwezo wa wananchi na hatimaye ukusanyaji wa mapato ya halmashauri.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Marco, amesema pamoja na changamoto hiyo, wilaya inaendelea kunufaika na sekta ya utalii, akisisitiza umuhimu wa kutumia fursa zilizopo kuongeza mapato na kuchochea maendeleo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameielekeza Halmashauri ya Serengeti kubuni vyanzo vipya vya mapato vinavyoendana na mahitaji ya sasa badala ya kuendelea kutegemea vyanzo vya jadi pekee.
Kanali Mtambi amesema utofauti wa uchumi unapaswa kwenda sambamba na ubunifu katika ukusanyaji wa mapato ili kuongeza uwezo wa halmashauri kugharamia miradi ya maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.
Discussion
Reader comments
0 contributions