Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa, amewahakikishia wananchi wa Kata ya Kamagambo wilayani Karagwe kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafiri na usafirishaji, hatua inayolenga kuchochea shughuli za kiuchumi na kuunganisha vijiji na kata mbalimbali.
Bashungwa ametoa kauli hiyo, alipokutana na Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kamagambo, katika mwendelezo wa ziara yake ya kikazi jimboni yenye lengo la kutoa mrejesho wa utekelezaji wa shughuli za Serikali na kusikiliza kero za wananchi.

Akizungumza katika kikao hicho, Bashungwa alisema Serikali imefanikiwa kuboresha barabara kadhaa ambazo awali zilikuwa katika hali mbaya, zikiwemo barabara za Nkwenda–Kafunjo–Nyabiyonza, Kafunjo–Kiregete na Kafunjo–Kijumbura, hatua ambayo imeongeza urahisi wa usafiri na usafirishaji wa bidhaa na huduma.
Aidha, alieleza kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Nyakahanaga–Kashada–Bushangaro kwa kiwango cha lami, ambapo kazi ya uwekaji lami katika maeneo korofi tayari imeanza huku matengenezo ya kawaida yakiendelea katika sehemu ambazo bado hazijafikiwa na lami.

Mbunge huyo pia alisema Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za Igombe–Rwenkorongo (Sokoni) na Busecha–Achikona, ambazo ni muhimu katika kuboresha mawasiliano na shughuli za maendeleo ndani ya Kata ya Kamagambo.
Katika sekta ya nishati, Bashungwa aliishukuru Serikali kwa kufanikisha upatikanaji wa umeme katika vijiji vyote vya kata hiyo, akibainisha kuwa hatua inayofuata ni kusambaza huduma hiyo katika vitongoji vyote. Alisema mkandarasi tayari ameanza kazi katika vitongoji vya Rwenkorongo na Igombe.

Kuhusu huduma ya maji, Bashungwa alisema amepokea changamoto zinazowakabili wananchi wa vitongoji vya Busecha na Rwenkorongo, akieleza kuwa maeneo hayo yatafanyiwa usanifu ili yaunganishwe na Mradi Mkubwa wa Maji wa Rwakajunju, utakaosaidia kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama.
Discussion
Reader comments
0 contributions