Skip to main content

SAFARI UTAFUTAJI HAKI KWA WANANCHI WENYE UWEZO MDOGO YAANZA KATAVI

Na Daniel Gahu – Katavi.

SAFARI UTAFUTAJI HAKI KWA WANANCHI WENYE UWEZO MDOGO YAANZA KATAVI

Na Daniel Gahu – Katavi.

Mwananchi mwenye kipato cha chini anapokutana na mgogoro wa ardhi, mirathi au ndoa, mara nyingi changamoto yake haishii kwenye kutafuta haki pekee, bali huanza na swali la ataipataje huduma ya kisheria bila kuwa na uwezo wa kugharamia wakili?

Hili ni miongoni mwa maswali ambayo sasa Mkoa wa Katavi umeanza kuyatafutia majibu, baada ya kuzindua Kamati za Kudumu za Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa na Wilaya pamoja na Kliniki ya Sheria bila malipo.

Kliniki hiyo imezinduliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuf, aliyemwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, ikiwa na lengo la kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi, hususan wale wasiokuwa na uwezo wa kugharamia huduma za mawakili.

Kwa mujibu wa viongozi, moja ya malengo makubwa ya kamati hizo ni kusaidia kupunguza mlundikano wa mashauri ya kisheria, huku wananchi wakipata ushauri na msaada katika masuala mbalimbali ikiwemo migogoro ya ardhi, mirathi, ndoa na changamoto nyingine za kisheria.

Hatua hii inakuja wakati ambapo wananchi wengi, hasa wenye kipato cha chini, wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya gharama za kupata huduma za kisheria, hali inayoweza kuwafanya kuchelewa au kushindwa kabisa kufuatilia haki zao.

Kwa wananchi waliohudhuria uzinduzi huo, huduma hii si jambo la kawaida, bali ni fursa inayoweza kubadilisha namna wananchi wanavyofikia haki.

Mmoja wa wananchi hao, Fortunate Kabeja, amesema gharama za mawakili zimekuwa miongoni mwa vikwazo vikubwa kwa wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria, hivyo uwepo wa kliniki hiyo unaweza kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo kwa wakati na kwa ukaribu.

Kwa mtazamo wake, nguvu ya kliniki hiyo itaonekana zaidi pale itakapoweza kushughulikia migogoro ambayo imekuwa ikigusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Anazitaja migogoro ya ardhi, ndoa na mirathi kuwa miongoni mwa changamoto zinazohitaji kupewa kipaumbele, kwa kuwa zimekuwa zikiathiri familia na mahusiano ya kijamii katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Katavi.

Ni kuona kama huduma hii itafika kwa mwananchi wa kawaida anayekabiliwa na mgogoro, lakini hana fedha za kumlipa wakili; kama ushauri utatolewa kwa wakati; na kama kamati hizi zitaweza kusaidia kupunguza migogoro inayoweza kutatuliwa kabla haijageuka kuwa mashauri marefu mahakamani.

Kwa Katavi, Kliniki ya Sheria bila malipo sasa imefungua ukurasa mpya wa kusogeza huduma za haki karibu na wananchi.

Changamoto iliyopo ni kuhakikisha ukurasa huo hauishii kwenye uzinduzi, bali unageuka kuwa huduma halisi inayomfikia mwananchi mwenye uhitaji, kwa wakati na bila kikwazo cha gharama.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.