Na Saada Almasi, Lamadi - Simiyu.
Katika kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Ujuzi kwa Vijana inayoadhimishwa Julai 15 ya kila mwaka Jambo Fm inakukutanisha na kijana Sadock Emmanuel mkazi wa Lamadi wilayani Busega mkoani Simiyu ambaye amekuwa mfano kwa kuwatoa tongotongo vijana wenzie baada ya kufanya ubunifu wa kutengeneza jiko ambalo linatumia mafuta machafu ya pikipiki ambayo humwagwa wakati wa kufanya matengenezo ya pikipiki kutokana na kutokuwa na matumizi tena.
Jiko hilo ambalo hufanya kazi kwa kumimina kiasi kidogo cha mafuta machafu katika eneo maalum kisha kuunganisha na nishati ya umeme kwa ajili ya kuzungusha feni inayo puliza na kuchochea moto kuwaka linauwezo wa kupika chakula cha aina yoyote kwa kutumia kiasi kidogo cha mafuta na kuokoa uchafuzi wa mazingira unaotiokea kila mafuta chafu yanapomwagwa ardhini.

Akizungumza na Jambo FM Sadock amesema kuwa jambo lililomsukuma kufanya ubunifu huo ni changamoto za ukosefu wa ajira zilizompa msukumo wa kusaidia vijana wenzie kupata kipato ambapo alibaini maeneo mengi mazingira yanaharibiwa huku serikali ikifanya juhudi kubwa kuhamasisha utunzaji wake huku vichafuzi vya mazingira vikiwa malighafi zinazoweza kutumika.
“Niliona kuna fursa kubwa katika kubadili changamoto inayokumba mazingira yetu ili yawe salama,maeneo ya ofisi za mafundi wa pikipiki ardhi imebadilika ni nyeusi na hata upande mti usitegemee ukakua hapo ndipo nilipopata wazo la kuleta ubunifu huu ili kuokoa mazingira na kuongeza kupato,” amesema Sadock.

Ameongeza kuwa kwa mtu ambaye anauwezo wa kumiliki jiko hilo nafuu atajiepusha na gharama kubwa za kununua mkaa kupikia na kuokoa gharama za umeme pamoja na muda kwani lita moja ya mafuta machafu ambayo kwa sasa yanapatikana bila malipo unauwezo wa kutumia wiki nzima kwa vyakula vya aina zote.
Kutokana na hilo Sadock anajiona ni championi wa kuokoa mazingira hasa katika ukataji wa miti hovyo kwa ajili ya kupata kuni kupikia hali ambayo inampa ushiriki wa moja kwa moja na wahifadhi wa wanyamapori TAWA katika kupiga vita uvamizi wa watu katika mapori ya akiba kukata miti kwa ajili ya matumizi mbalimbali

“Kwanza teknolojia iliyotumika ni rahisi na kutumia haya mafuta machafu tunaokoa mazingira mara nyingi wananchi wanaingia katika migogoro na wahifadhi wa wanyama mpori hasa waliokandokando na hifadhi kutokana na kuingia porini na kuchukua kuni kwa kukata miti sasa yakiwepo majiko haya huo muingiliano wa wanyama na binaadamu tunakwenda kuumaliza.”
Lusato Masinde askari wa wanyama pori kutoka TAWA akizungumza na wakazi wa Lamadi katika uzinduzi wa jiko hilo diwani wa kata hiyo Joseph Goryo ameutaka uongozi wa TAWA kujitoa kununua majiko hayo na kuyagawa kwa wananchi ili wananchi waone kwa vitendo dhamira yao ya kulinda misitu na wanyama bila kuathiri shughuli za kibinaadamu.

“Mmekuwa mkishiriki shughuli nyingi za kimaendeleo kwa wananchi ikiwepo msaada wa madawati, kujenga shule kuchangia bati zahanati na mengineyo ninaamini haya majiko mkiyanunua na kuwagawia wananchi huko vijijini kama mnavyofanya,"
"Kwenye miradi mingine mtatoa hamasa kwa vitendo juu ya utunzaji wa mazingira kwa sababu hawa wananchi ukiwapelekea wanaamini zaidi kuliko ukiwaambia na hiyo itapunguza migongano kati yenu huko katika hifadhi,” amesema Joseph Goryo Diwani wa kata ya Lamadi.
Discussion
Reader comments
0 contributions