Na, Adam Msafiri - Mara.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara imesema rushwa ni miongoni mwa sababu zinazochangia uharibifu wa mazingira kwa kuruhusu vitendo vya ukataji miti na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za asili kuendelea kufanyika katika jamii.
Akizungumza katika shughuli za uhamasishaji wa utunzaji wa mazingira, Afisa wa TAKUKURU Mkoa wa Mara, Agness Taratibu amesema, mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira hayawezi kufanikiwa bila ushirikiano wa wananchi, viongozi na taasisi mbalimbali katika kusimamia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Wakati huo huo,baadhi ya wakazi wa mkoa wa Mara,wameeleza wasiwasi wao kuhusu kuendelea kwa matumizi ya kuni na miti katika uchomaji wa matofali, wakisema hali hiyo inachangia kupungua kwa uoto wa asili na kuharibu mazingira.
Wakazi hao, akiwemo George Tole, Amos Chacha na Faustina Silvester, wamependekeza matumizi ya pumba za mpunga kama mbadala wa kuni katika uchomaji wa matofali ili kupunguza kasi ya ukataji miti na kulinda mazingira.

Katika hatua nyingine, juhudi za kuhamasisha utunzaji wa mazingira zimeendelea kufanyika mashuleni kupitia utoaji wa elimu kwa wanafunzi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira na matumizi sahihi ya rasilimali za asili.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Butata, Mwl. Nyamta Wanga amesema elimu hiyo imekuwa ikiwajengea wanafunzi uelewa wa kutunza mazingira tangu wakiwa wadogo, huku mwanafunzi Sister Emerda Dickson akieleza kuwa elimu wanayoipata imewasaidia kutambua wajibu wao katika kulinda mazingira.

Wadau wa mazingira wanaendelea kusisitiza kuwa ushiriki wa jamii, taasisi za serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Discussion
Reader comments
0 contributions