Vikosi vya Jeshi la upinzani vya Rapid Support Forces (RSF) nchini Sudan vimefanya shambulio la ndege zisizo na rubani (drones) dhidi ya kituo kikuu cha umeme katika mji mkuu wa Khartoum.
Shambulio ambalo limeongeza msukosuko wakati jamii ya kimataifa ikitoa onyo kali kuhusu janga la njaa linalotishia mamilioni ya raia katika Taifa hilo lililoko kaskazini mashariki mwa Africa.
Afisa mwandamizi wa shirika la umeme la grid ya Taifa nchini Sudan, aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alithibitisha kuwa droni za RSF zilishambulia kituo cha kubadilisha umeme cha Al-Markhiyat siku ya Jumanne.
"Droni za kundi la RSF zimeshambulia kituo cha Al-Markhiyat na kusababisha kukatika kwa umeme katika maeneo makubwa ya majimbo ya Khartoum na Al-Jazira," alisema afisa huyo
Shambulio hilo linajiri ikiwa ni siku moja tu baada ya operesheni nyingine iliyoandaliwa na RSF kushambulia vituo sita vya umeme na kusababisha giza nene katika majimbo manne mashariki mwa Sudan.
Umoja wa Mataifa (UN) umeonya mara kadhaa kuwa mashambulizi dhidi ya miundombinu ya umeme yanahatarisha huduma za afya na maisha ya mamilioni ya watu.
Tangu mwezi Aprili 2023, Sudan imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya RSF chini ya Mohamed Hamdan Dagalo na jeshi la serikali chini ya Jenerali Abdel Fattah al-Burhan linalodhibiti maeneo ya katikati, kaskazini, na mashariki mwa nchi.
Mashirika ya msaada yanakadiria kuwa vita hivyo vimeshaua zaidi ya watu 200,000 na kusababisha mzozo mkubwa zaidi wa wakimbizi na njaa duniani.

Wakati huo huo, Marekani, Umoja wa Ulaya (EU), na nchi zaidi ya 30 zimetoa onyo kali kuhusu "kuzorota kwa kutisha" kwa usalama wa chakula nchini Sudan, zikitaka hatua za haraka kuchukuliwa ili kuzuia janga la njaa.
Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani siku ya Jumatatu, mataifa yaliyosaini ikiwemo Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Kanada, na Australia yamezitaka pande zinazopigana kuondoa vizuizi vyote vya misaada ya kibinadamu.

"Sudan inashuhudia kuzorota kwa kutisha kwa usalama wake wa chakula. Hatari ya njaa katika miezi ijayo, kama ilivyoonywa na Mfumo wa Ainisho ya Hatua za Usalama wa Chakula (IPC), inahitaji hatua za haraka," ilieleza taarifa hiyo. "Pande zinazopigana ndizo zenye dhamana kuu ya kupunguza mateso ya wananchi wa Sudan."
Discussion
Reader comments
0 contributions