Na Gideon Gregory- Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amewaelekeza watumishi wa umma katika nafasi zao kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa uwazi, uaminifu, weledi na ufanisi ili kuepusha mararamiko kwa wananchi na serikali.
Ridhiwani ametoa maelekezo hayo leo Juni 17,2026 wakati akifungua maonesho Wiki ya Utumishi yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma yanayokwenda sambamba na kauli mbiu isemayo “kuchochea uwajibikaji jumuishi kwa huduma endelevu”.

"Wafanyakazi wetu ndiyo msingi wa maendeleo yetu, mkitimiza wajibu wenu mafanikio makubwa na maendeleo tunayoyataka kama Watanzania tutayafikia," amesema.
Aidha, amewakumbusha waajiri wote katika taasisi za umma kuhakikisha kuwa zinawapatia mafunzo waajiri wapya mafunzo ya awali pale punde wanapoajiriwa ili waweze kufahamu na kuishi tamaduni inayokubalika katika utumishi wa umma.

"Serikali inasisitiza kuendelea kutoa mafunzo ya awali kwa watumishi wapya ili kuwaandaa katika utekelezaji wa majukumu yao na kuwapa elimu kuhusu majukumu yanayopaswa kutekelezwa kwenye masuala ya maadili, sheria, taratibu na kanuni mbalimbali zinazosimamia utumishi wa umma"ameongeza.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi amesema jumla ya taasisi 225 zinashiriki katika maonesho hayo ya Wiki ya Utumishi wa Umma likiwa ni ongezeko kutoka taasisi 146 zilizoshiriki mwaka 2025.

Amesema maadhimisho hayo yanaambatana na maonesho ya shughuli mbalimbali za Serikali yatakayodumu hadi Juni 23, mwaka huu, yakitoa fursa kwa wananchi kupata huduma na taarifa kutoka taasisi mbalimbali za umma.
Amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea maonesho hayo ili kupata huduma mbalimbali za Serikali pamoja na kufahamu shughuli zinazotekelezwa na taasisi hizo.
Discussion
Reader comments
0 contributions