Kocha wa Real Madrid, José Mourinho, ameendeleza ubabe wake katika michezo ya El Clásico baada ya kuiongoza timu yake kupata ushindi muhimu wa mabao 2-1 dhidi ya Barcelona katika uwanja wa Camp Nou, matokeo yaliyofufua ushindani wa kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania, La Liga.
Mchezo huo umemshuhudia mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa, Kylian Mbappé akifunga mabao yote mawili ya Real Madrid, likiwemo bao la ushindi dakika za mwisho, na kuhitimisha rekodi ya Barcelona ya kushinda michezo tisa ya mwanzo ya ligi msimu huu.

Ushindi huo umepunguza tofauti ya pointi kati ya Barcelona na Real Madrid kutoka sita hadi tatu, huku miamba hiyo ya Hispania ikiendelea kupambana katika mbio za kuwania ubingwa wa msimu wa 2026/2027. Ushindi huo ulikuwa wa kipekee kwa Mourinho, ambaye amerejea kuinoa Real Madrid baada ya miaka 13.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 63 alishindwa kuficha furaha yake baada ya bao la ushindi la Mbappé, akiteleza kwa magoti karibu na eneo la benchi la ufundi katika shangwe zilizowakumbusha mashabiki namna alivyokuwa akisherehekea ushindi katika kipindi chake cha kwanza Madrid.
Kwa matokeo hayo, Mourinho amekuwa kocha wa tatu katika historia ya Real Madrid kuiongoza timu hiyo katika michezo sita mfululizo ya El Clásico bila kupoteza, akiwa na ushindi mara nne na sare mbili.
Rekodi hiyo imemweka katika kundi moja na makocha wa zamani wa Real Madrid, Miguel Muñoz aliyefanya hivyo kati ya mwaka 1962 na 1965, pamoja na Vicente del Bosque kati ya mwaka 2001 na 2003.
Katika mazungumzo yake baada ya mchezo, Mourinho alisisitiza kwamba lengo kubwa la Real Madrid si kushinda mchezo mmoja dhidi ya Barcelona pekee, bali kutwaa ubingwa wa La Liga.
Alieleza kuwa kikosi chake kilicheza kwa utulivu na nidhamu kubwa, huku akiwapongeza wachezaji kwa kufanya kazi kwa pamoja na kutekeleza maelekezo ya kiufundi. Mourinho pia alisisitiza umuhimu wa kutobweteka baada ya ushindi huo, akieleza kwamba timu yake inapaswa kuendeleza kiwango hicho katika michezo inayofuata.

Kwa upande wa Barcelona, kocha Hansi Flick alikiri kwamba wachezaji wake hawakuwa na nguvu za kutosha kutokana na ratiba ngumu ya michezo katika wiki za karibuni.Flick amesema hana nia ya kutafuta visingizio vya kipigo hicho lakini alisisitiza umuhimu wa wachezaji wake kupata muda wa kurejesha nguvu na kujiandaa vizuri kwa michezo inayofuata.
Barcelona iliingia katika El Clásico ikiwa imeshinda michezo yote tisa ya mwanzo ya La Liga, hivyo ushindi mwingine ungeifanya kuweka rekodi mpya ya kushinda michezo 10 ya mwanzo wa msimu wa ligi hiyo hata hivyo Real Madrid iliizuia kufikia rekodi hiyo na kuipa Barcelona kipigo chake cha kwanza cha ligi msimu huu.
Ushindi wa Real Madrid unatengeneza utofauti mdogo wa alama ambapo kwa sasa Bacelona bado anaongoza ligi akiwa na alama 27 huku Real Madrid ana akiwa nafasi ya tatu na alama 24 kibindoni jambo linalozifanya mbio za ubingwa kuendelea kuwa mvuto mkubwa zaidi na kuzilazimu timu zote kushinda mechi zote zilizopo mbele yao.
Discussion
Reader comments
0 contributions