Na Tryphone Odace - Kigoma.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro amewataka wataalamu kutoka taasisi mbalimbali kushirikiana kwa karibu na mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) Lot 7 na 8 kutoka Uvinza hadi Msongati nchini Burundi ili kubaini na kuondoa vikwazo vinavyoweza kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo.
Lengo la kikao hicho ni kupokea taarifa ya maendeleo ya usanifu wa awali wa mradi wa ujenzi wa reli hiyo na kuweka mikakati ya pamoja kati ya taasisi za umma zinazohusika na utekelezaji wa mradi katika Mkoa wa Kigoma.

Akizungumza leo wakati wa kikao hicho, Balozi Sirro amesema ni muhimu kwa mkandarasi kufanya kazi kwa ushirikiano na watendaji wa Serikali pamoja na kuwashirikisha wananchi katika hatua zote muhimu za utekelezaji wa mradi, ili kufahamu mahitaji yao na kupunguza malalamiko yasiyo ya lazima wakati wa ujenzi na baada ya mradi kukamilika.
Aidha, Balozi Sirro amesisitiza kuwa watendaji wote kutoka nje ya Tanzania wanaoshiriki katika mradi huo kuheshimu sheria, kanuni na taratibu za nchi, pamoja na kuepuka vitendo vya ukatili, ubaguzi na unyanyasaji dhidi ya wananchi wa Tanzania.

Kwa upande wao, wajumbe wa kikao hicho wameshauri kuwa changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi mingine ya SGR nchini zitumike kama funzo ili zisijirudie katika ujenzi wa Lot 7 na 8, unaotarajiwa kupita katika Wilaya za Uvinza, Kasulu na Buhigwe Mkoani Kigoma.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, zikiwemo TANROADS, TARURA, TFS, Idara ya Ardhi, RUWASA na TANESCO ngazi ya Mkoa, ambao wanashiriki katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa mradi huo
Discussion
Reader comments
0 contributions