Na Tryphone Odace - Kigoma.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amevitaka vyama vya ushirika kuwa waadilifu na kuhakikisha wakulima wananufaika na zao la tumbaku, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa mkoa.
Balozi Sirro ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha Bodi ya Tumbaku kilichowakutanisha wadau wa zao hilo kwa ajili ya kujadili na kutafuta suluhu ya changamoto zinazowakabili wakulima.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa katika kikao hicho, tumbaku ni miongoni mwa mazao yanayochangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa Mkoa wa Kigoma ambapo katika msimu wa 2025/2026, zao hilo lilishika nafasi ya pili kwa kuchangia zaidi ya shilingi bilioni 5 katika pato la mkoa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Dinna Mathamani, amesema viongozi wanapaswa kuelekeza nguvu katika kutoa elimu kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na kuboresha tija ya zao hilo.
“Unajua kama wakulima wetu hawatapata elimu sahihi ya kilimo cha tumbaku uzalishaji hauwezi kuwa na tija kwani unakuta wanalima eneo kubwa lakinianajikivuna hakiendani na ukubwa shamba sasa nadhani ni muda wa sisi viongozi kutoa elimu kwa wakulima wetu” amesema Mathamani.
Kwa upande wake, Afisa Mazingira wa Bodi ya Tumbaku, Elisha Chao, amesema Tanzania imezalisha tumbaku yenye thamani ya dola za Marekani milioni 475 katika msimu wa kilimo wa 2024/2025.

Amesema bodi hiyo inaendelea kuchukua hatua dhidi ya wanunuzi wasio waaminifu, ikiwa ni pamoja na kutowapa leseni, ili kuhakikisha wakulima wananufaika zaidi na zao hilo.
Akitoa maelekezo kwa viongozi wa Bodi ya Tumbaku na vyama vya ushirika, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma amesisitiza umuhimu wa kuweka mifumo itakayomhakikishia mkulima kupata manufaa stahiki kutokana na kilimo cha tumbaku.
Aidha, amewataka wakulima kuzingatia taratibu za ukataji wa miti wanapohitaji kuni kwa ajili ya kukausha tumbaku, akisisitiza umuhimu wa kulinda mazingira.

Zao la tumbaku ni miongoni mwa mazao makuu ya biashara katika Mkoa wa Kigoma na huwapatia kipato wakulima wengi, hususan katika wilaya za Kasulu, Kakonko na Uvinza.
Hata hivyo, wakulima wa tumbaku wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kushuka kwa bei ya zao hilo na upatikanaji wa pembejeo, hali inayohitaji ushirikiano wa karibu kati ya serikali, vyama vya ushirika, bodi na wadau wengine wa sekta hiyo.
Discussion
Reader comments
0 contributions