Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amekabidhi msaada wa vifaa na mahitaji mbalimbali ya kibinadamu kwa wakazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji walioathiriwa na mvua kubwa zilizoambatana na upepo mkali zilizonyesha mkoani humo siku kadhaa zilizopita.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Balozi Sirro amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya athari za mvua, ikiwemo kuondoka katika maeneo ya mabondeni na maeneo mengine hatarishi ili kulinda maisha na mali zao.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simo Sirro, Picha na Tryphone Odace
Amesema wananchi wanapaswa kuzingatia masuala ya usafi wa mazingira kwa kuepuka kutupa taka ovyo, akieleza kuwa tabia hiyo huchangia kuziba kwa mitaro ya maji na kusababisha maji kuingia katika makazi ya watu.
“Ni muhimu wananchi kuchukua tahadhari, hasa wale wanaoishi maeneo ya mabondeni, wahakikishe wanahama katika maeneo hayo ili kuepusha madhara yanayoweza kusababisha kupoteza maisha,” amesema Sirro.
Aidha, amewaelekeza wakurugenzi wa halmashauri kupitia Kamati za Maafa kuendelea kufuatilia hali za wananchi walioathiriwa na mvua na kuhakikisha wanapatiwa msaada unaohitajika kulingana na mahitaji yao.

“Kamati za Maafa ziendelee kufuatilia wananchi waliokumbwa na maafa haya na kuhakikisha wanapata msaada unaostahili. Pia, nitoe pongezi kwa uongozi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa hatua ya kutoa misaada hii kwa wananchi,” amesisitiza Sirro.
Kwa upande wake, akitoa taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Hashim Mvogogo, amesema halmashauri imetoa jumla ya tani 2.6 za mchele, tani 1.95 za unga, kilo 910 za maharage, kilo 390 za sukari pamoja na kilo 390 za sabuni ya unga.
Amesema mahitaji mengine yaliyotolewa ni lita 650 za mafuta ya kupikia, maturubai 260, mashuka 260, mablanketi 260 pamoja na magodoro 260, kwa ajili ya kuwasaidia wananchi waliopoteza au kuathiriwa na makazi yao.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simo Sirro akikaidhi msaada huo, Picha na Tryphone Odace
Mvogogo amesema tathmini iliyofanyika imebaini kuwa jumla ya nyumba 121, makanisa manne yaliyojengwa kwa miti pamoja na ghala moja vimeathiriwa na mvua hizo.
Ameongeza kuwa watu wawili walijeruhiwa kutokana na mvua zilizoambatana na upepo mkali, ambapo mmoja tayari ameruhusiwa kutoka hospitalini huku mwingine akiendelea kupata matibabu.
Hatua ya utoaji wa msaada huo inalenga kuwasaidia waathirika kukabiliana na changamoto za kibinadamu zilizosababishwa na mvua hizo huku mamlaka zikiendelea kusisitiza umuhimu wa tahadhari na usafi wa mazingira ili kupunguza athari za mafuriko.
Discussion
Reader comments
0 contributions