Na Ibrahim Rojala, Mbogwe - Geita.
Ukosefu wa huduma ya Nishati ya Umeme na Maji Safi na Salama umetajwa kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazoikabili Shule ya Sekondari Bunigonzi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, mkoani Geita.
Diwani wa Kata ya Bunigonzi, Sylivester John Ntugwa, ameeleza hayo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, aliyefika shuleni hapo kukagua mradi wa ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu mbalimbali. Kutokana na changamoto hizo, Mkuu wa Mkoa alitaka ufafanuzi kutoka kwa mamlaka husika kuhusu hatua zinazochukuliwa kuzitatua.

Katika miradi hii ambayo umeitembelea kuna changamoto mbalimbali,tuna changamoto ya umeme,shule hii ikiwezeshwa umeme,waalimu wanadai kwamba kuna uwezekano wa shule hii kuwa ya kwanza kimkoa kwenye habari ya matokeo kwenye mitihani,mheshimiwa mkuu wa mkoa tunaomba sana,lakini changamoto ya pili tena maji,tunavyo vyoo vya kisasa ,wanafunzi wanapata shida sana,wanalazimika kuja na maji”ameeleza Ntugwa
Akizungumzia suala la upatikanaji wa maji, Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mbogwe, Judith Mndende, amesema tayari kisima kimechimbwa katika Kijiji cha Bunigonzi na kwamba hatua za upembuzi zinaendelea ili kuhakikisha huduma ya maji inafikishwa katika taasisi zote zilizopo ndani ya kijiji hicho, ikiwemo shule hiyo.

Kwa upande wa umeme, Meneja wa TANESCO Wilaya ya Mbogwe, Mhandisi Fabian Rukiko, amesema shule zote ndani ya wilaya hiyo ambazo bado hazijafikiwa na huduma ya umeme zimeingizwa katika mpango wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Ameongeza kuwa kiasi cha shilingi milioni 45 kinahitajika ili kufikisha huduma ya umeme katika Shule ya Sekondari Bunigonzi.
Kufuatia maelezo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, amemtaka Meneja wa TANESCO Wilaya ya Mbogwe kuendelea kufuatilia upatikanaji wa fedha hizo ili mradi wa umeme utekelezwe haraka, aidha, ameagiza huduma ya maji kufikishwa katika shule hiyo kabla ya Desemba 25, 2026.

“Kwenye shule ambazo nimetembelea,hii ni miongoni mwa shule nzuri ambazo zinapendeza,hata ukiangalia tiles zake zimekaa vizuri,nimeenda kwenye mabweni super kabisa na kwakweli tutaweka msukumo tuweze kuleta umeme ili watoto wetu waishi hape kwenye mabweni,wasome hata usiku kwasababu miundombinu ipo”amesema RC Shigela
Mradi wa ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu katika Shule ya Sekondari Bunigonzi umehusisha ujenzi wa bweni moja la wasichana, ukamilishaji wa vyumba viwili vya madarasa, maabara tatu, jengo moja la utawala, jengo moja la Tehama pamoja na jengo moja la maktaba.

Utekelezaji wa mradi huo umegharimu jumla ya shilingi 267,154,712.50 zilizotolewa na Serikali Kuu, Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), huku wananchi wakichangia shilingi 5,800,000 kupitia nguvu zao za maendeleo.


Discussion
Reader comments
0 contributions