Na Ibrahim Rojala - Geita.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela, ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Bukombe kubuni na kutekeleza miradi mipya ya kuongeza mapato, badala ya kuendelea kutegemea mapato yatokanayo na madini peke yake.
Ametoa maagizo kupitia kikao maalum cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichoketi kusikiliza na kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2026.

Aidha RC Shigela amewataka madiwani kuacha tabia ya kutengeneza hoja ili zijibiwe, na badala yake kuzuia mapungufu kabla hayajatokea ili kuitunza taswira ya Serikali.
Akizungumza kwa niaba ya madiwani,mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Bukombe,Erick Kagoma, amesema amepokea na atatekeleza maelekezo ya kupunguza idadi ya hoja zinazoibuliwa na CAG katika miaka ijayo.

Katika hatua nyingine halmashauri ya wilaya ya Bukombe imepongezwa kwa kufanikiwa kupata hati safi katika ukaguzi wa CAG ambapo kwa mujibu wa ripoti ya CAG, jumla ya hoja 24 ziliibuliwa kwa mwaka 2026 ndani ya halmashauri hiyo, hadi sasa hoja tano kati ya hizo zimepatiwa majibu wakati hoja 19 zikiendelea kufanyiwa kazi.
Aidha halmashauri hiyo imefanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni 5 fedha ambazo ni mapato ya ndani ikiwa ni sawa na asilimia 136.3 ya makusanyo ikilinganishwa na lengo ililojiwekea.






Discussion
Reader comments
0 contributions