Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti, ameitaka Manispaa ya Geita kuharakisha ukamilishaji wa uwanja wa mpira wa miguu wa Magogo ili uanze kutumiwa na wananchi kwa shughuli za michezo na burudani.
Mnyeti ametoa agizo hilo Jumanne, Oktoba 13, 2026, alipokagua maendeleo ya mradi huo uliopo Mtaa wa Magogo,kata Manispaa ya Geita, huku akishauri halmashauri kutumia wataalamu wake na taasisi za Serikali kupunguza gharama za ujenzi.
Pia Mnyeti amesema kwa uzoefu alioupata alipotembelea Shule ya Wasichana ya Nyankumbu hivi karibuni ulimfanya kutambua umuhimu wa kuwa na maeneo salama na yanayofaa kwa shughuli za kimichezo zilizo tofauti na shule.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti akiwa katika eneo la Magogo Manispaa ya Geita mahali ambapo Mradi wa Ujenzi wa Uwanja wa mpira wa miguu unaendelea kutekelezwa.
Aidha ameshauri juu ya umuhimu wa kutumia wakandarasi wa ndani kwa kazi ambazo zimekuwa zikifanywa kampuni binafsi ikiwemo za nje ya nchi badala ya kutumia wahandisi wa Serikali waliopo ndani ya halmashauri, akizitaka mamlaka husika kuangalia uwezekano wa kushirikisha wazawa kupunguza gharama.
“Watu wetu lazima wajue kwamba wanawajibika kwa Serikali, ikiwa ni pamoja na kutumia akili zao walizonazo ndiyo maana wakawa wahandisi. Sasa, mhandisi wetu una kazi gani kwenye Manispaa yetu kama vitu vidogo kama hivi huwezi kuvijenga? Hivi kujenga majukwaa tu hapa mnahitaji mpaka mkandarasi? Mpaka mzabuni?” amehoji Mnyeti.

Ramani ya uwanja wa mpira wa miguu unaotakiwa kujengwa katika eneo la Magogo halmashauri ya Manispaa ya Geita.
Ujenzi wa uwanja huo ni miongoni mwa miradi miwili ya kimkakati ambayo Baraza la Madiwani la Manispaa ya Geita, katika kikao chake cha Agosti 21, 2026, liliazimia kusitisha mikataba yake baada ya changamoto za utekelezaji kujitokeza.Mradi huo uliokwama ukiwa asilimia 75, ulikuwa ukitekelezwa kwa ufadhili wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR), kabla ya kukwama kutokana na mvutano wa muda mrefu kati ya halmashauri na mgodi huo.
Mkurugenzi mtendaji wa Manispaa ya Geita, Yefredi Myenzi, amesema awali SUMA JKT ilipewa mkataba wa Shilingi milioni 163.38 kwa ajili ya kusawazisha eneo na kufanya kazi za awali huku mkataba ukitekelezwa kwa miezi mine,hata hivyo mkataba huo ulisitishwa baada ya Mkandarasi kushindwa kukamilisha kazi hiyo kulingana na mkataba huku akiwa tayari amelipwa zaidi ya Shilingi milioni 25.
Kutokana na uwepo wa changamoto hiyo,halmashauri chini ya Mhandisi wa Mkoa iliamua kutafuta mkandarasi mwingine ambaye ni M/S EFQ Company limited and Mugoo Construction Limited ili kuendeleza ujenzi huo uliofikia Shilingi bilioni 2.6 ikiwemo ushuru wa ongezeko la thamani(VAT),ambao nao ulisitishwa Septemba 20,2023 huku mkandarasi akiwa tayari amelipwa zaidi ya Shilingi bilioni 2.17.
Mwaka 2023 Serikali kupitia Wizara ya madini ilifanya mabadiliko ya kanuni za utekelezaji wa miradi ya CSR ambapo mmiliki wa leseni alipewa jukumu la kutafuta mkandarasi kutekeleza miradi ya CSR hivyo Manispaa kusitisha mkataba na kampuni hiyo,kufuatia mabadiliko hayo,Kampuni ya GGML ilipewa jukumu la kuajiri mkandarasi kukamilisha mradi,takwa ambalo liliendelea kuleta mivutano na kukwamisha ujenzi kuendelea.

Mwonekano wa namna mpangilio wa Majukwaa utakvyokuwa pindi uwanja wa mpira wa miguu unaojengwa katika eneo la Magogo,Manispaa ya Geita utakapokamilika.
Mradi husika unahusisha ujenzi wa eneo la kuchezea mpira, njia za riadha, uzio, miundombinu ya maji safi, jukwaa kuu, vyumba vya kubadilishia nguo pamoja na vyoo.
Pia uwanja huo unahusisha ujenzi wa majukwaa matano ya watazamaji yenye uwezo wa kuchukua watu 5,000, huku kila jukwaa likiwa na nafasi ya watazamaji 1,000,ukitarajiwa kuwekwa nyasi bandia, hatua ambayo Mnyeti ameshauri halmashauri kuanza taratibu za kuziagiza mapema ili utaratibu wa kuziombea msamaha wa kodi uanze.
Kwa upande wake, Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Geita, Elias Ngole, amesema matarajio ya wananchi kuhusu kukamilika kwa uwanja huo yako mbioni kutimia baada ya changamoto zilizokwamisha utekelezaji kuanza kutatuliwa.
“Matamanio ya wananchi sasa yanakwenda kukamilika, na sisi tunawaahidi kwamba kufikia mwezi wa pili, uwanja huu unakwenda kukamilika, kwani sintofahamu zilizokuwepo ni kama tumezikamilisha,” amesema.
Aidha ujenzi wa Uwanja huo unatarajiwa kuanza mwendelezo wake tena kuanzia Novemba 06, 2026 baada ya mkandarasi kupatikana huku ukitakiwa kukamilika baada ya miezi mitatu ifikapo Februari 06, 2027.
Discussion
Reader comments
0 contributions