Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amekutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Kamanda wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Magharibi, Ndugu Ali Maggid, ofisini kwake iliyopo Manispaa ya Shinyanga.
Kikao hicho kililenga kujadili masuala mbalimbali yanayohusu uhifadhi wa misitu, utunzaji wa mazingira pamoja na namna ya kukabiliana na changamoto zinazoathiri rasilimali za misitu ndani ya Mkoa wa Shinyanga.

Akizungumza mara baada ya mazungumzo hayo, RC Mhita amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha usimamizi wa misitu na mazingira kwa kushirikisha wananchi pamoja na taasisi zote zinazohusika na uhifadhi wa maliasili.
Amesema Mkoa wa Shinyanga unaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kulinda mazingira ikiwemo kuhamasisha upandaji miti, kudhibiti uharibifu wa misitu pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Uhifadhi wa misitu ni jukumu la kila mmoja wetu. Tunapaswa kushirikiana kuhakikisha tunalinda rasilimali hizi muhimu ambazo ni msingi wa maisha na maendeleo ya wananchi wetu,” amesema Mhita.
Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa TFS Kanda ya Magharibi, Ali Maggid, amesema ziara yake ofisini kwa Mkuu wa Mkoa ilikuwa ni sehemu ya kujitambulisha rasmi baada ya kupata nafasi hiyo, pamoja na kujadili namna bora ya kuendeleza ushirikiano kati ya TFS na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa katika kusimamia masuala ya uhifadhi.

Aidha, ameeleza kuwa TFS itaendelea kushirikiana na viongozi wa serikali pamoja na wananchi katika kuhakikisha misitu inalindwa dhidi ya uharibifu unaotokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu.
Mazungumzo hayo pia yaligusia umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi sahihi ya rasilimali za misitu, kudhibiti ukataji holela wa miti pamoja na kuimarisha mikakati ya uhifadhi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Shinyanga.

Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa maeneo yanayoendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya utunzaji wa mazingira na upandaji miti ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha uwepo wa mazingira endelevu kwa maendeleo ya jamii.
Discussion
Reader comments
0 contributions