Na Eunice Kanumba - Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amelipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kwa mafanikio makubwa katika kupunguza matukio ya uhalifu, hatua inayochangia kuimarika kwa amani na usalama wa raia na mali zao.
RC Mhita ametoa pongezi hizo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Familia ya Polisi (Police Family Day) yaliyofanyika katika Manispaa ya Shinyanga, akieleza kuwa kazi inayofanywa na jeshi hilo ni muhimu kwa ustawi wa jamii.

“Niwapongeze Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kwa kuendelea kuonesha weledi na kujituma katika kupunguza uhalifu. Hali hii imeimarisha amani na usalama wa wananchi. Nawahimiza muendelee kushirikiana na jamii ili kudumisha hali hiyo,” amesema RC Mhita
Aidha, amewakumbusha askari hao kuendelea kuonesha uzalendo, kufanya kazi kwa bidii na kuweka maslahi ya taifa mbele, huku wakidumisha umoja na mshikamano katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, alisema Siku ya Familia ya Polisi inalenga kuimarisha mshikamano kati ya askari, familia zao na jamii kwa ujumla, pamoja na kuthamini mchango wao katika kudumisha amani.
Maadhimisho hayo yamepambwa na shughuli mbalimbali ikiwemo ukaguzi wa gwaride, maonesho ya mbinu za ukamataji wahalifu kwa kutumia mbwa maalum, gwaride la singe, pamoja na ugawaji wa tuzo kwa askari waliofanya vizuri katika mwaka 2025.

Discussion
Reader comments
0 contributions