Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Beno Malisa amemuapisha Christopher Andendekisye Kitwika kuwa Mkuu wa Wilaya ya Uyui, katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mtemi Isike Mwanakiyungi, Manispaa ya Tabora.
Akitoa salamu za Mkoa baada ya uapisho huo, RC Malisa amemtaka DC Kitwika kumheshimisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, kutatua kero za wananchi na kushirikiana na viongozi wa Chama na Serikali katika kuwaletea maendeleo.
“Na kumuheshimisha Rais ni kazi ndogo sana, katimize Majukumu yako, Basi..! hamna cha sijui umpelekee Rais mchele, la hasha, wewe timiza tu majukumu yako, tatua kero za wananchi wako,” amesisitiza RC Malisa.
Aidha, amemsihi Mkuu huyo wa Wilaya kuzuia migogoro katika eneo lake la kazi na kutumia wasaidizi wake pamoja na Kamati ya Usalama ya Wilaya kutatua na kuepusha migogoro.
Amemtaka pia kufanya kazi kwa weledi huku akiheshimu mila na desturi za wananchi wa Uyui na Mkoa wa Tabora kwa ujumla.
Kwa upande wake, akitoa salamu baada ya kula kiapo cha Uongozi na Maadili, Kitwika amewashukuru viongozi wa Chama na Serikali waliohudhuria hafla hiyo na kuomba ushirikiano wao katika kutekeleza majukumu yake.
Kitwika ameahidi kushirikiana na viongozi hao katika kuwatumikia wananchi wa Wilaya ya Uyui na kufanikisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Discussion
Reader comments
0 contributions