Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, ameongoza Kamati ya Siasa ya Mkoa katika ukaguzi wa miradi minne ya maendeleo, akisisitiza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unapaswa kwenda sambamba na malengo ya Dira ya Taifa 2050.
Miradi iliyokaguliwa ni pamoja na Soko la Kimataifa la Vitunguu, Jengo la Wazazi katika Hospitali ya Sokonine, Shule ya Msingi Mwakiteo pamoja na Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Singida.
Akizungumza wakati wa majumuisho ya ziara hiyo, Dendego amesema miradi hiyo ni sehemu ya hatua zinazoweka msingi wa kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2050, hivyo shughuli za maendeleo zinapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia mwelekeo wa Dira hiyo.
“Tunapoendelea kutekeleza miradi ya maendeleo, ni muhimu kuhakikisha kila hatua inaendana na maelekezo na malengo ya Dira ya Taifa 2050,” amesema .
Aidha, amesema Soko la Kimataifa la Vitunguu lina nafasi ya kuwa miongoni mwa maeneo yanayoweza kuvutia wageni na kuchangia kukuza utalii wa Mkoa wa Singida, kutokana na umuhimu wake katika shughuli za biashara na kilimo cha vitunguu.
Katika hatua nyingine, Dendego amesisitiza umuhimu wa kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuwaunganisha na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali, akieleza kuwa fursa hizo zinapaswa kuwafikia vijana na kusaidia kuongeza shughuli za uzalishaji.
Pia ametoa wito wa kuchukuliwa hatua dhidi ya ukataji holela wa miti ya asili, huku akihimiza maandalizi ya mapema kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño zinazotarajiwa.
Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Singida imehitimisha ziara yake iliyozishirikisha Wilaya zote za Mkoa huo iliyolenga kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwa wananchi.
Discussion
Reader comments
0 contributions