Na Saulo Stephen - Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amewaelekeza viongozi wote wa Serikali na madiwani kutumia vikao vyao, kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa mipango ya maendeleo, ukusanyaji wa mapato, ulipaji wa madeni na kufungwa kwa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ndani ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani cha kujibu hoja za CAG kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Dendego ameipongeza halmashauri hiyo kwa kukusanya zaidi ya asilimia 103 ya mapato ya ndani na kupata hati safi kwa miaka 12 mfululizo.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa mafanikio hayo yawe chachu ya kubuni vyanzo vipya vya mapato, kuongeza kasi ya utekelezaji wa Dira ya 2050 na kuhakikisha wastani wa kipato cha mwananchi unaongezeka kwa kasi kupitia uwekezaji na matumizi bora ya rasilimali zilizopo.
Amesema viongozi wanapaswa kuisoma, kuielewa na kuitafsiri Dira ya 2050 katika bajeti, mipango na maamuzi ya kila siku, akibainisha kuwa maendeleo ya wananchi yatachangiwa na ongezeko la mapato, usimamizi wa fedha za umma na uwezeshaji wa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa wa Singida amesisitiza kuwa watakaozalisha hoja mpya za ukaguzi watawajibishwa, huku akimtaka Mkuu wa Wilaya kuhakikisha kila mwezi utekelezaji wa Dira ya 2050 na maendeleo ya kufunga hoja unajadiliwa rasmi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Juma Mwanga, amesema madiwani watahakikisha maagizo yote yaliyotolewa yanatekelezwa, ikiwemo kufunga hoja za ukaguzi, kusimamia urejeshaji wa mikopo ya asilimia 10 na kuongeza uwajibikaji katika kata zote ili halmashauri iendelee kufanya vizuri.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson, amesema uongozi wa wilaya hautavumilia uzalishaji wa hoja mpya za CAG na watakaozalisha watachukuliwa kama alivyoelekeza Mhe. Dendego.
Discussion
Reader comments
0 contributions