Na Saulo Stephen - Singida.
Katika kuhakikisha majanga hayakatishi huduma za elimu, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, ametembelea Shule ya Seminari Diagwa iliyopo Mughanga, Makuro, Halmashauri ya Wilaya ya Singida, iliyopata janga la kuungua kwa majengo mawili, akisisitiza kuwa watoto lazima waendelee kupata elimu.
Akizungumza shuleni hapo, Dendego ameshukuru kwa jitihada zilizofanyika kwa kuwa hakuna mwanafunzi aliyepoteza maisha katika tukio hilo na kueleza kuwa Serikali imefika hapo kutoa pole, kusikiliza changamoto na kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama kubaini chanzo cha moto, ili matukio kama hayo yasijirudie.

Aidha, Dendego amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na Mbunge imetoa msaada wa magodoro 35, kilo 200 za mchele, kilo 100 za sukari, lita 40 za mafuta ya kupikia, sabuni na mashuka vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 2 kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi walioathirika.
Dendego amesisitiza kuwa Serikali itashirikiana na kanisa katoliki kuhakikisha majengo yaliyoteketea yanajengwa upya kwa haraka ili wanafunzi waendelee kupata elimu katika mazingira salama.

Vilevile, amewapongeza wananchi, Kanisa, Jeshi la Zimamoto na vyombo vya ulinzi na usalama kwa ushirikiano mkubwa walioonyesha wakati wa kukabiliana na janga hilo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe, amesema tayari kamati ya wataalamu imeundwa kuchunguza chanzo cha moto na inatarajiwa kukamilisha ripoti yake ifikapo Julai 17, 2026. Amesema wilaya itaendelea kushirikiana na wananchi na vyombo vya usalama kuhakikisha mazingira ya shule yanakuwa salama na huduma za elimu zinaendelea bila usumbufu.

Aidha uongozi wa shule umeeleza kuwa moto uliharibu mabweni mawili, sehemu ya kanisa, ghala pamoja na chumba cha mlezi wa mabweni, huku wanafunzi wote, wakiwemo watahiniwa 42 wa Darasa la Saba, wakinusurika na kuhamishiwa katika seminari nyingine ya Kanisa Katoliki kuendelea na maandalizi ya mtihani wao. Uongozi huo umeishukuru Serikali, wananchi na Jeshi la Zimamoto kwa msaada walioutoa.


Discussion
Reader comments
0 contributions