Na Saulo Stephen - Singida.
Katika maandalizi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego akiwa ameambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Singida, amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotarajiwa kutembelewa, kuzinduliwa na kuwekwa jiwe la msingi na Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri za Wilaya za Manyoni na Itigi.
Ukaguzi huo ulianza Wilaya ya Manyoni ambapo kamati ilikagua Uwanja wa Shule ya Msingi Tambukareli utakaotumika kupokea Mwenge wa Uhuru kutoka Wilaya ya Itigi.

Miradi mingine iliyokaguliwa ni mradi wa vijana wa utengenezaji wa samani uliopo Mang'oni wenye thamani ya shilingi milioni 15.7, mradi wa nishati safi katika Shule ya Sekondari Mwanzi, mradi wa sekta binafsi wa ujenzi wa hoteli ya kisasa eneo la Kipondoda pamoja na mradi wa maji wa visima 10 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Solya.
Katika Wilaya ya Itigi, kamati hiyo ilikagua Kituo cha Afya Idodyandole, Mradi wa Maji Mbugani, mradi wa elimu katika Shule ya Sekondari Itigi utakaohusisha ugawaji wa madawati na uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi, mradi wa vijana wa MULUCAN Group ulionufaika na mkopo wa asilimia 10 wa Halmashauri wenye thamani ya shilingi milioni 12.

Mwingine ni mradi wa miundombinu wa Songambele, uwekezaji wa sekta binafsi wa ghala la minada ya dengu pamoja na ujenzi wa Ofisi ya Kijiji cha Mlowa unaotekelezwa kwa nguvu za wananchi. Aidha, walikagua eneo la Stendi ya Zamani ya Itigi ambalo litatumika kwa mkesha wa Mwenge wa Uhuru.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Dendego amewataka viongozi kuendelea kufanya ziara za mara kwa mara katika hospitali, vituo vya afya na zahanati ili kufuatilia ubora wa huduma na kupunguza malalamiko ya wananchi. Pia amesisitiza umuhimu wa kuwapatia vikundi vya vijana fursa za kazi kupitia miradi ya Halmashauri ili kuimarisha urejeshaji wa mikopo ya asilimia 10.

Aidha, amewahimiza vijana kutumia fursa za mikopo inayotolewa na Serikali kujenga miradi yenye tija, kuongeza ajira na kuwa chachu ya maendeleo katika jamii. Vilevile, amesisitiza suala la usafi wa mazingira katika maeneo yote ya miradi.

Discussion
Reader comments
0 contributions