Na Saulo Stephen - Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, ameutaka uongozi wa Chemba ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC) Mkoa wa Singida kuongeza idadi ya wanachama kutoka 68 waliopo sasa na kufikia wanachama 1,000 ndani ya kipindi cha miezi mitatu ili kuimarisha umoja na fursa za kiuchumi kwa wanawake wafanyabiashara mkoani humo.
Dendego ametoa maelekezo hayo Juni 20, 2026 wakati wa maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa TWCC, yaliyofanyika katika ukumbi wa RC Social mjini Singida. Amesema ongezeko la wanachama litasaidia kuimarisha sauti ya wanawake wafanyabiashara, kuongeza ushiriki wao katika uchumi na kupanua fursa za biashara na uwekezaji.

Amesisitiza kuwa TWCC ina nafasi kubwa ya kuwaunganisha wanawake katika shughuli za maendeleo na kuwawezesha kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotolewa na Serikali pamoja na taasisi nyingine za maendeleo.
Katika hatua ya kuonyesha dhamira yake ya kuunga mkono jitihada hizo, Dendego amesema yuko tayari kuwa mwanachama wa 1,000 mara tu lengo hilo litakapofikiwa ndani ya muda uliowekwa.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Katibu wa TWCC Mkoa wa Singida, Rosemary Ibrahim, amesema uongozi wa chemba hiyo umejipanga kutekeleza maelekezo ya Mkuu wa Mkoa kwa kuhakikisha idadi ya wanachama inaongezeka na kufikia lengo lililowekwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu.
Rosemary amesema katika kuhamasisha wanawake wengi zaidi kujiunga, TWCC imetoa ofa maalum ambapo wanachama binafsi watajiunga kwa ada ya shilingi 50,000 zinazoweza kulipwa kwa awamu ndani ya miezi mitatu ya kampeni hiyo. Aidha, kwa vikundi na kampuni, ada ya kujiunga itakuwa shilingi 100,000.

Kwa upande wake, Afisa Biashara Mkoa wa Singida, Donatila Vedasto, amepongeza uongozi wa TWCC Mkoa wa Singida pamoja na wanachama wake kwa kuadhimisha miaka 20 ya chemba hiyo, akieleza kuwa hatua hiyo inaonyesha uthubutu, mshikamano na mchango mkubwa wa wanawake katika shughuli za ujasiriamali na maendeleo ya uchumi.
Amesema wanawake wafanyabiashara wameendelea kuwa nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Singida na taifa kwa ujumla, huku akiwahimiza kuendelea kutumia TWCC kama jukwaa la kukuza biashara zao, kubadilishana uzoefu na kutafuta masoko ya bidhaa na huduma zao.

Maadhimisho hayo yamewakutanisha viongozi wa Serikali, wafanyabiashara wanawake na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa lengo la kutathmini mafanikio ya TWCC katika kipindi cha miaka 20 na kujadili mikakati ya kuimarisha ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi.
Discussion
Reader comments
0 contributions