Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha ameongoza viongozi wa serikali, maofisa wa Jeshi la Polisi pamoja na mamia ya wananchi katika shughuli ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, SACP Richard George Abwao.
Hafla hiyo imefanyika katika Viwanja vya FFU Tabora ambapo waombolezaji wamekusanyika kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu kabla ya mwili wake kusafirishwa kwenda Mkoa wa Mara kwa ajili ya mazishi.

Akizungumza katika shughuli hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Chacha amesema kifo cha SACP Abwao ni pigo kubwa kwa Jeshi la Polisi na Mkoa wa Tabora kutokana na mchango wake mkubwa katika kuimarisha usalama na utulivu wa wananchi.
Amesema "Marehemu alikuwa kiongozi mwenye nidhamu, aliyefanya kazi kwa weledi na kujituma katika kutekeleza majukumu yake."

Mwili wa marehemu uliwasili mkoani Tabora usiku wa kuamkia leo ukitokea mkoani Morogoro na kupokelewa na viongozi wa serikali, maofisa wa Jeshi la Polisi pamoja na wananchi waliokuwa wamejitokeza kwa wingi.
Baada ya shughuli za kuaga mwili kukamilika, mwili wa SACP Richard George Abwao unatarajiwa kusafirishwa jioni ya Leo kuelekea Wilaya ya Rorya mkoani Mara ambako marehemu anatarajiwa kuzikwa katika kijiji cha Shirati, ambako familia, ndugu, jamaa na wananchi wataungana kumpumzisha katika nyumba yake ya milele.




Discussion
Reader comments
0 contributions