
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Rogath Mboya, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, ameiongoza Kamati ya Usalama Mkoa kukagua miradi 13 yenye thamani ya jumla ya Sh bilioni 4.29 itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 katika Halmashauri za Wilaya za Kaliua na Urambo.
Katika ziara hiyo, Dkt. Mboya ameambatana na wajumbe wa Kamati ya Usalama Mkoa pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Katika wilaya ya Kaliua, Kamati imekagua jumla ya miradi sita yenye thamani ya Sh bilioni 1.82, ikiwemo ujenzi wa Barabara ya Usinge kwa kiwango cha lami, mradi wa maji katika Kijiji cha Usinge, ujenzi wa Ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Ugansa na vyumba sita vya madarasa katika Shule ya Sekondari Ugansa. Miradi mingine ni kikundi cha vijana wa Bodaboda Igagala na ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Ugunga, huku wilaya ya Urambo, Kamati kamati imekagua miradi saba yenye thamani ya Sh bilioni 2.47 ikiwemo ujenzi wa nyumba ya mganga katika Zahanati ya Uhuru na vyumba sita vya madarasa Shule ya Sekondari Kasisi.

Baada ya ukaguzi huo, Kamati imewapongeza wasimamizi na watekelezaji wa miradi iliyozingatia vigezo vya Mwenge wa Uhuru, sheria na taratibu za ununuzi wa umma pamoja na ubora unaoendana na thamani ya fedha zilizotolewa huku kamati hiyo ikiwataka kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ambayo haijakamilika bila kuathiri viwango na ubora wa kazi.

Dkt. Mboya pia amewakumbusha wasimamizi wa miradi kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Kamati, huku wakihakikisha nyaraka zote muhimu zinakamilishwa, zinapangwa na kuhifadhiwa kwa usahihi.
Pia amewahimiza viongozi na wananchi wa Kaliua na Urambo kuhamasika na kujitokeza kwa wingi kuupokea, kuukimbiza na kuienzi falsafa ya Mwenge wa Uhuru.
Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuwasili Tabora Septemba 15, 2026 ukiwa na ujumbe unaosisitiza kuthamini na kudumisha amani kwa maendeleo ya Taifa. “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo.”
Discussion
Reader comments
0 contributions