Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Fatuma Mganda ameeleza kutoridhishwa na hali ya usafi katika maeneo ya barabara za Makongoro - Airport na barabara za mjini kati, akisema maelekezo yaliyotolewa awali hayajatekelezwa kikamilifu. Dkt. Mganda ameyasema hayo Novemba 3, 2026 wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya usafi katika maeneo hayo ambapo amebaini kuwepo kwa mapungufu yanayohitaji hatua za haraka.
Kutokana na hali hiyo, amewataka Maafisa Afya wa Wilaya za Nyamagana na Ilemela kuongeza usimamizi na kuhakikisha maelekezo ya usafi yanatekelezwa ipasavyo katika maeneo yao. Amesema usimamizi dhaifu ndio chanzo cha kuendelea kuwepo kwa uchafu licha ya maelekezo ya mara kwa mara kutoka kwa uongozi wa Mkoa.

Aidha, amewataka wananchi wanaoishi pembezoni mwa barabara hizo kuwajibika kwa kusafisha maeneo yanayowazunguka badala ya kusubiri kukumbushwa au kutegemea wafanyakazi wa usafi. Amesema kila mwananchi ana wajibu wa kuutunza mazingira yake ili mji uwe safi na wenye kuvutia.
Vilevile, amewataka mawakala waliopewa mikataba ya kufanya usafi barabarani kutekeleza majukumu yao kwa viwango vinavyotakiwa, akisisitiza kuwa mikataba hiyo lazima iendane na matokeo yanayoonekana. Amewataka kutofanya kazi kwa mazoea bali kuhakikisha barabara zinabaki safi wakati wote.

Katika kuhamasisha uwajibikaji, Dkt. Mganda ameshiriki na kuonesha kwa vitendo namna ya kufanya usafi katika baadhi ya kaya zilizopo pembezoni mwa barabara hizo. Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuendeleza utaratibu wa kufanya usafi mara kwa mara bila kusubiri viongozi kufika katika maeneo yao, kwani mazingira safi yanahitaji uwajibikaji wa kila mmoja. Ameeleza kuwa usafi wa mazingira ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano kati ya viongozi, wananchi na wadau wote wanaohusika ili kuhakikisha maeneo ya barabara yanakuwa safi na yanavutia wakati wote.
Discussion
Reader comments
0 contributions