Skip to main content

RAMA ADAKWA AKIHUJUMU MIUNDOMBINU YA TANESCO KATAVI

Na Daniel Gahu - Katavi.

RAMA ADAKWA AKIHUJUMU MIUNDOMBINU YA TANESCO KATAVI

Na Daniel Gahu - Katavi.

Katika tukio linalozua wasiwasi kuhusu usalama wa miundombinu ya umeme nchini, kijana mmoja mwenye umri wa miaka 27, aliyetambulika kwa jina la Ramadhani Shaha Seleman, mkazi wa Kata ya Ilembo, Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, amekamatwa na wananchi kwa tuhuma za kuharibu na kuiba nyaya za shaba katika transfoma inayomilikiwa na Shirika la Umeme Tanzania, TANESCO.

Tukio hilo limetokea katika Kata ya Kabungu, Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, ambapo kwa mujibu wa mashuhuda, mtuhumiwa anadaiwa kuanza kutekeleza vitendo hivyo tangu tarehe 15 Julai. Hata hivyo, jitihada za awali za kumkamata hazikufanikiwa hadi viongozi wa kijiji na kata walipoandaa mkakati maalum wa doria za usiku kwa kushirikiana na wananchi.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Bi. Lusia Mtema Jilala, amesema kuwa ushirikiano wa wananchi ndio uliowezesha kukamatwa kwa mtuhumiwa akiwa anadaiwa kuendelea kukata nyaya za shaba kutoka kwenye transfoma.

"Nilimuona kwa kumchungulia nikiwa ndani ya nyumba, ndipo nikawasiliana na Mtendaji wa Kijiji. Alikusanya vijana haraka, wakamzingira na kufanikiwa kumkamata akiwa bado eneo la tukio." amesema Bi Lusia.

Baada ya kukamatwa, wananchi wa eneo hilo wamezitaka mamlaka husika kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake ili tukio hilo liwe fundisho kwa wengine wanaoweza kujihusisha na uharibifu wa miundombinu ya umeme.

Wananchi hao wamesema vitendo vya aina hiyo vinaweza kusababisha hasara kubwa kwa Serikali pamoja na kuwaathiri wakazi wa kijiji kwa kukosa huduma muhimu ya umeme ambayo imekuwa kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Kata ya Kabungu, Bi. Ziada Mnahahe, amesema mafanikio ya kukamatwa kwa mtuhumiwa yametokana na ushirikiano mzuri kati ya viongozi na wananchi.

Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na kuwataka vijana kujihusisha na shughuli halali za kujipatia kipato badala ya kujihusisha na vitendo vinavyoharibu mali za umma.

Katika mahojiano baada ya kukamatwa, mtuhumiwa alikiri kuhusika na kitendo hicho, akidai kuwa alichukua hatua hiyo kutokana na madai yake kwamba anaidai TANESCO Mkoa wa Katavi kiasi cha shilingi milioni mbili na laki mbili kwa kazi alizowahi kufanya chini ya shirika hilo, fedha ambazo anasema hajalipwa.

Hata hivyo, madai hayo hayathibitishi au kuhalalisha uharibifu wa miundombinu ya umma, na mamlaka husika zinatarajiwa kuendelea na uchunguzi pamoja na taratibu za kisheria ili kubaini ukweli wa tukio hilo na hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.