Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Dangote Group, Alhaj Aliko Dangote, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Dangote, ambaye ni mwekezaji na mfanyabiashara kinara barani Afrika, amezungumzq na Rais Samia hii leo Juni 28, 2026 na kueleza utayari wa kampuni yake kupanua ushirikiano wa uwekezaji na Serikali katika sekta mbalimbali za kimkakati.

Mazungumzo hayo yamegusa maeneo ya miundombinu ya usafirishaji, uzalishaji wa
mbolea nchini na nishati, kama sehemu ya fursa za uwekezaji zinazoweza kuchochea shughuli za kiuchumi nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Dangote amesema, Tanzania ina mazingira mazuri ya uwekezaji na fursa kubwa za kukuza
viwanda vinavyoongeza thamani ya malighafi na kuchochea biashara ya kikanda.

"Tumetambua maeneo yenye manufaa makubwa kwa Tanzania na tuko tayari
kushirikiana na Serikali kuyaendeleza kwa manfaa ya pande zote," amesema Dangote.
Kwa upande wake, Rais Dkt. Samia amesema Serikali imepokea nia hiyo na kuzielekeza
wizara na taasisi husika kuendelea na majadiliano ya kitaalamu kuhusu maeneo
yaliyojadiliwa, kwa kuzingatia sera, sheria na vipaumbele vya maendeleo ya nchi.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuvutia uwekezaji wenye
tija unaochochea ukuaji wa uchumi, maendeleo ya viwanda, uhamishaji wa teknolojia na
ajira kwa Watanzania.

Discussion
Reader comments
0 contributions