Na Gideon Gregory - Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itatenga fedha maalumu zitakazowezesha Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kuzipatia mitaji kampuni changa zinazomilikiwa na vijana (startups), ili ziweze kukua na kushindana katika soko la kidigitali.
Amesema hayo leo Aprili 10, 2026 Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi ya minara 758 na maunganisho ya mkongo wa mawasiliano katika wilaya 85 pamoja na kukabidhi mkongo wa mawasiliano serikalini.
“Tutatenga fedha zitakazoiwezesha Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kuzipatia mitaji kampuni changa za vijana (startups) ili ziweze kukua zaidi,” amesema.
Ameongeza kuwa uwekezaji katika sekta ya Tehama ni muhimu kwa mustakabali wa uchumi wa taifa, hasa katika kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha huduma za kidigitali katika sekta mbalimbali.

Sambamba na hayo, ameziagiza mamlaka zinazohusika kuhakikisha huduma za mawasiliano zinazotolewa nchini zinazingatia maadili, mila na tamaduni za Kitanzania, akisisitiza kuwa kukosekana kwa udhibiti kunaweza kuathiri malezi na uzalendo wa kizazi cha sasa.
Katika eneo hilo, Rais Samia ameeleza kufurahishwa na mpango wa kampuni ya Huawei ambao wamemueleza kuhusu utengenezaji wa mfumo wa Akili Unde (AI) wa Kiswahili kwa ajili ya Watanzania, utakaosaidia kulinda maadili ya jamii.
“Nikuombe Waziri shirikiana nao kwa karibu ili wakamilishe mapema. Vijana wetu wakipata mfumo huu, kiwango cha ubunifu kitaongezeka. Vijana wa Kitanzania wana ubunifu mkubwa sana, hata bila mafunzo ya kompyuta wanafanya kazi kubwa ndani ya mifumo ya kidijitali,” amesema Rais Samia.
Kwa upande wake Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema licha ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa minara 758 pamoja na kuimarishwa kwa minara 304, Serikali bado inaendelea kutekeleza miradi mingine ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za mawasiliano za uhakika.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Mwasalyanda, amesema kuwa mwaka 2023 mfuko huo ulikabidhiwa jukumu la utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758, pamoja na kuiongezea nguvu minara 304 kutoka teknolojia ya 2G kwenda teknolojia ya 3G na 4G.
Amesema utekelezaji wa mradi huo umefanyika kwa ushiririkiano kati ya Serikali kupitia UCSAF na watoa huduma ya mawasiliano ya simu nchini, ambapo Serikali ilitoa ruzuku ili kuchochea uwekezaji katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.
Discussion
Reader comments
0 contributions