Mtoto mmoja mwenye umri wa miaka 11, Aishara Shingu, ambaye alikuwa akisoma darasa la sita katika Shule ya Msingi Ussoke, Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, amefariki dunia baada ya kupigwa na radi huku watu wengine watano wakijeruhiwa.
Akizungumza na waandishi na habari hapo jana Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tabora, Loshipay Laizer, ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea wakati mvua kubwa ikiendelea kunyesha. Waathirika walikuwa shambani wakifanya shughuli zao za kila siku kabla ya kukimbilia kujikinga chini ya mti.

Kwa mujibu wa Laizer, hatua ya kujificha chini ya mti ndiyo iliyowaweka katika hatari, kwani radi iliwapiga wakiwa hapo. Mtoto huyo alipoteza maisha papo hapo, huku wengine wakipata majeraha mbalimbali.
Majeruhi wa tukio hilo wametajwa kuwa ni Mamula Shingu (43), Marando Shingu (24), Danale Rungole (21), Pumbula Mango (29) pamoja na Tungu Masanja (41), ambao kwasasa wanapatiwa matibabu katika vituo vya afya vya Wilaya ya Urambo.
Discussion
Reader comments
0 contributions