Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Bi. Rabia Abdallah Hamid, amewataka wataalamu wa Serikali wenye majukumu ya kuwahudumia wananchi kutoka ofisini na kwenda katika maeneo ya wananchi ili kubaini changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.
Bi. Hamid ameyasema hayo mkoani Tabora wakati wa ziara yake yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kusikiliza kero za wananchi na kujionea namna Serikali inavyowahudumia.
Katika ziara hiyo, Bi. Hamid amezungumza na viongozi wa Chama na Serikali, watumishi wa umma, wanachama wa CCM pamoja na wawakilishi wa makundi mbalimbali ya wananchi katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Tabora Polytechnic.
Amesema maafisa wa Serikali wenye majukumu ya kuwafikia wananchi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa vitendo, ikiwamo kutembelea maeneo husika, kubaini changamoto na kuchukua hatua za kuzitatua.
“Maafisa wa Serikali wenye majukumu ya kwenda maeneo ya wananchi wafanye hivyo na wawasilishe taarifa zinazoonesha maeneo waliyotembelea, vikundi walivyovisaidia, wananchi waliokutana nao, changamoto walizobaini na hatua walizochukua kuzitatua,” amesisitiza Bi. Hamid.
Aidha, amewahimiza watu wenye ulemavu kutokujiona wanyonge wala kubaki nyuma katika kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotolewa na Serikali, ikiwamo mikopo isiyo na riba inayotolewa na halmashauri.
Bi. Hamid amesema wapo watu wengi wenye ulemavu ambao wametumia fursa hizo kuanzisha shughuli za uzalishaji na kukuza mitaji yao, hivyo kuwataka wengine kutumia fursa zinazopatikana kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Beno Malisa, amewataka wataalamu wa kada mbalimbali kutoa majibu ya kina kwa hoja, maswali na kero zinazowasilishwa na wananchi.
RC Malisa pia amekemea uzembe unaofanywa na baadhi ya watumishi wa umma pamoja na matumizi ya lugha zisizo na staha kwa wananchi wanapofika katika ofisi za Serikali kupata huduma.
“Tuendelee kujikita katika kutatua kero za wananchi. Kila halmashauri iwe na siku maalumu ya kusikiliza na kutatua kero zao,” amesema RC Malisa.
Discussion
Reader comments
0 contributions