Na Ibrahin Rojala - Geita.
Jua kali la mchana linawaka katika Kata ya Nyawilimilwa wilayani Geita ndaniyamkoawa Geita, pembeni katika moja kati ya nyumba zinazopatika katika eneo maarufu la Carlfonia anaonekana akiwa amesimama punda mmoja ambaye mguu wake wa mbele wa kushoto umejikunja ikiwa ni matokeo ya ajali ya kugongana na pikipiki iliyomsababishia ulemavu na kwasasa hawezi tena kutembea kama zamani.
Licha ya kuwa na majeraha yaliyosababishwa na ajali mwili wake umenakshiwa na alama za makovu na vidonda vilivyoanza kukauka,mmiliki wake,Mashaka Motomkali anaeleza kwamba ajali iliyompata punda wake ilimgharimu kiasi cha shilingi 300,000 zilizotumika katika matibabu lakini hata hivyo punda huyo haweza kufanya kazi tena!
‘Kwenye kazi hafanyi kazi yoyote,sasa hivi simtumii nitaona hadi atakapopona, ikishindikana basi atabaki nyumbani,lakini punda hawa wamekuwa wakinisaidia kufuata mihogo,mahindi,kuni kwaajili ya matumizi ya hapa nyumbani’, anasema Motomkali.

PUNDA: NGUZO YA MAENDELEO KWA BAADHI YA FAMILIA
Wakati mfugaji huyu akiugulia hasara,kuna wengine punda wao wamewaboreshea maisha akiwemo Jofrey Juma Pamba (27),mkazi wa kitongoji cha Mtinanchi Nyawilimilwa aliyeanza kufuga punda mwaka 2017 baada ya kuamua kuachana na shughuli ya uvuvi.
Kilichomsukuma kuhamia katika ufugaji wa punda ni fursa alizoziona katika sekta ya ujenzi kama vila mahitaji ya mawe na mchanga katika kata hiyo ambayo inakua kwa kasi,mahitaji ya vifaa vya ujenzi yakiwa makubwa,anaeleza kwamba awali punda wake walipitia changamoto mbalimbali kutokana na kutokuwa na uelewa wa matunzo yake.
‘Kile kipindi wakati naanza kuwafanyisha kazi nilikuwa sijui namna ya kuwapumzisha, ila kwa sasa hivi naenda nao vizuri sina changamoto yoyote na wanyama wangu,elimu hii niliipata kupitia uzoefu tu kwenye kazi yangu kwahiyo nikatambua kuwa kwa mafanikio waliyonipa ni muhimu nikawajali na kuwapumzisha,inapofika saa nne ninawapumzisha mpaka kesho tena,” anasema Pamba.

Pamba anasema punda wamemsaidia kupata viwanja viwili na ng’ombe sita akieleza kwamba mtu akitaka kumkwaza basi awaseme vibaya punda kwasababu anajua walikomtoa mpaka walipomfikisha na kuomba uwepo wa umoja wa wamiliki wa punda katika kata yao hatua anayoeleza kuwa itaimarisha zaidi mapato yao na mustakabali wa ustawi wa punda.
SAFARI YA MATESO NA MAFANIKIO
Masimango kutoka kwa watu aliokuwa akiwafanyia vibarua na hali ngumu ya maisha vililimkalisha chini Bwana Masanja Edward na kutafakari mno kabla ya kupata wazo la kufuga punda,ndipo alianza na punda mmoja ambaye kwa maelezo yake anadai kuwa alimnunua akiwa amechoka hali iliyomlazimu kumtibu na kumtunza kabla ya kununua punda wa pili na kuanza kuwafanyisha kazi.
Moja kati ya jambo ambalo hawezi kulisahau ni kumpoteza mmoja kati ya punda wake aliyekufa kutokana na uzembe wa kukosa uangalizi wa kutosha akiwa malishoni.

“Yaani baada ya kifo cha yule punda niliumia sana,nilimaliza siku kama tatu nikiwa sili vizuri,baada ya hapo anapokanyaga punda wangu ndipo ninapokanyaga mimi, maana kifo kile kilinifanya nijue punda ana thamani sana maana kazi nilizokuwa nafanya zikawa zimefeli kutoka tripu tano mpaka mbili au tatu kwa siku,’’ anabainisha Masanja
Kifo cha punda wake kilimuumiza na kumvunja moyo lakini halikumkatisha tama ndipo alipoamua kufunga safari ya kutoka Mkoani Geita hadi Singida kununua punda wawili.
“Baada ya kununua punda nilianza safari ya kutembea kwa mguu kutoka Singida kurudi Geita,nilitembea wiki mbili na siku nne kufika Nyawilimilwa,njiani nilipigwa mvua,kulala kwenye mitaro,lakini nikaendelea na safari mpaka nilipofika na mpaka leo wapo na wanaendelea na kazi,’ anaeleza Masanja.

Akizungumzia faida ya punda anabainisha kwamba amendokana na manyanyaso ya kufanya vibaru kwa watu,kupata fedha za haraka ambapo kwa siku hakosi fedha kuanzia Shilingi 20,000 na pia wamekuwa wakimsaidia fedha zinazotumika katika shughuli za shambani hivyo amendokana na kilimo cha jembe la mkono.
Akizungumzia faida ya punda anabainisha kwamba amendokana na manyanyaso ya kufanya vibaru kwa watu,kupata fedha za haraka ambapo kwa siku hakosi fedha kuanzia Shilingi 20,000 na pia wamekuwa wakimsaidia fedha zinazotumika katika shughuli za shambani hivyo amendokana na kilimo cha jembe la mkono.
UKATILI DHIDI YA PUNDA UNAENDELEA
Licha ya yote hayo katika maeneo mbalimbali ya kata hii, baadhi ya punda wanaendelea kufanyishwa kazi kwa muda mrefu bila kupumzishwa,wengine wakipigwa au kubeba mizigo mizito kupita uwezo wao na kuachwa hata bila matibabu wanapoumwa.

Ni hali inayowaacha wakiwa na majeraha uchovu na wakati mwingine kupoteza kabisa uwezo wao wa kufanya kazi na mwisho kabisa hupoteza maisha.
Agness Onesmo ameeleza kuwa punda wana msaada katika kazi mbalimbali kama vile kuchota maji,kusomba kuni mchanga na matofali lakini kilio chake ni kuhusu mateso wanayopitia wanyama hao ikiwa ni pamoja na muda mrefu wa kufanya kazi,kupigwa wakiwa na vidonda licha ya kuwa wamekuwa na msaada mkubwa kwa wanawake wa Nyawilimilwa.
David Gideone Mmari anaona kuwa punda wana msaada mkubwa katika ujenzi lakini huzuni yake ni kuona wanyama hao wakinyanyasika kwa vipigo,kutokula kwa wakati na kupumzika akitaka viongozi wa serikali kuwajibika kwa kuwajengea uwezo wafugaji ili waweze kuwatendea haki.

SERIKALI INAFANYA NINI KUWAOKOA PUNDA?
Afisa Mifugo wa Kata ya Nyawilimilwa Joyce Sonza Kiruvuko ameeleza kwamba kata hiyo ina punda wasiopungua 120 ambao wamekuwa wakisaidia shughuli mbalimbali za kijamii,wakikabiliwa na changamoto ya kukosa haki zao na kukiri kwamba mnyama punda amekuwa akisahaulika hata katika chanjo zinazotolewa na serikali kwa wanyama mbalimbali.
“Tumefanya juhudi mbalimbali ikiwemo kuwa na vikao au mikutano na wamiliki wa hawa wanyama kazi vyamara kwa mara kuwakumbusha lakini pia kuwaelekeza namna wanavyopaswa kuwahudumia hawa wanyama punda na kuwatunza lakini pia kutimiza zile haki zao.” Amesema Joyce.
Anaeleza kuwa imewalazimu kutumia sheria kali na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kuwachukulia hatua ambao wamekuwa wakikiuka na kuongeza kuwa mara nyingi wanyama wamekuwa wakifanyishwa kazi wakiwa na majeraha,kufanyishwa kazi kwa zaidi ya masaa 8 hadi 10,kutopumzishwa na uwepo wa tabia ya kuwaachia watoto kazi ya kuswaga punda bila ya kuzingatia sheria wala usalama husuani wanapokuwa barabarani.

Afisa huyu wa serikali anasisitiza umuhimu wa punda kupumzishwa,kutibiwa wanapopata majeraha,kuwapunguzia muda wa kufanya kazi punda wenye mimba kutofanyishwa kazi ngumu na kutoa wito kwa wagugaji kuendelea kuwatunza punda ambao ni chanzo cha kipato katika kaya akieleza kuwa kwa kadri wanavyotunzwa ndivyo wanaweza kutumika kwa muda mrefu zaidi.
‘Waoge kwa wakati kwa kutumia dawa zinazohitajika, lakini pia matumizi dawa za minyoo mara kwa mara yanasaidia afya yake kwa ujumla kuwa katika hali nzuri”amesisitiza Joyce
TAKWIMU ZINAKATISHA TAMAA
Akizungumza hivi karibu katika warsha ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusiana na uchechemuzi na uandishi wa habari za utetezi wa haki za mnyama kazi punda mkoani Geita, Mkurugenzi wa shirika lisilo la Kiserikali la Arusha Society for the Protection of Animals (ASPA), Livingstone Masija alielezea umuhimu mkubwa wa wanyama hawa kwa binadamu na Binadamu na malengo ya maendeleo Endelevu (SDG’s).

Alisema tafiti zinakadiria kuwa wanyama kazi punda,farasi na jamii ya wanyama wengine katika kundi hilo wapatao milioni 100 duniani wana mchango katika shughuli za maendeleo hususani maeneo ya vijijini wakibeba mizigo,kushiriki katika shughuli za kilimo,ufugaji pamoja na kuhusika katika utafutaji wa maji.
Masija alibainisha kuwa mnyama kazi Punda wa pili kwa kuchangia pato la kaya kati ya wanyama wanaofugwa na binadamu hii ikiwa ni kwa mujibu wa Utafiti Uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TARILI).
Punda wa Tanzania wanapitia mengi kwani, Takwimu zilizowahi kutolewa na taasisi ya AIPWA zilieleza kuwa kila mwezi punda wapatao 150 kutoka Tanzania, huingizwa nchini Kenya kwa njia zisizo halali.

Hali hii inatishia kutoweka kwa wanyama hawa nchini licha ya Afrika kuwa na azimio la marufuku ya biashara ya punda kwa miaka 15, lilioasisiwa mwaka 2011, ili kutoa fursa ya wanyama hao kuendelea kuzaliana kutokana na punda kuwa na mzunguko mrefu wa uzazi unaoambatana na kipindi kirefu cha kubeba mimba takribani miezi 10 - 12 na kulea mtoto kwa muda mrefu hali inayopelekea uwepo wa idadi ndogo ya punda nchini.
Punda pia hawawezi kulalamika lakini wanabeba mizigo,wanabeba uchovu na wakati mwingine, wanabeba maumivu na hata kukata tama, hivyo inabaki kuwa wajibu wa kila mmoja kuhakikisha wanyama wanaotusaidia katika maisha ya kila siku wanatunzwa kwa utu na huruma.
Discussion
Reader comments
0 contributions