Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limetoa msaada wa vifaa mbalimbali, ikiwemo vifaa tiba, kwa wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kutokana na majeraha waliyopata kwa ajali za vyombo vya moto na kuvunjika sehemu mbalimbali za miili yao.
Hatua hiyo ni sehemu ya kuendeleza matendo ya huruma, kurejesha kwa jamii na kuunga mkono juhudi za kuwahudumia wenye uhitaji ambayo Jeshi la Polisi limekuwa likifanya katika makundi mbalimbali.
Akizungumza wakati wa kutoa msaada huo leo, Julai 27, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Wilbrod Mutafungwa amesema wamefika hospitalini hapo kwa ajili ya kuwaona na kuwafariji wagonjwa. Katika kuwafariji, wamewapelekea vitu mbalimbali vikiwemo vifaa tiba na kuwakatia wagonjwa hao bima za afya.

Fedha hizo ni sehemu ya michango kutoka kwenye mishahara ya maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali wa ndani ya Jeshi la Polisi mkoani wa Mwanza.
"Tunafurahi kwamba vitu hivi vimeweza kupokelewa kwa upendo mkubwa sana na uongozi wa Hospitali ya Bugando," amesema Kamanda Mutafungwa.
Jeshi la Polisi limekuwa na utaratibu wa kuyafikia makundi mbalimbali na kuyafariji kutokana na changamoto mbalimbali wanazopitia. Safari hii, wameamua kutembelea wodi ya wagonjwa waliopata ajali na kuvunjika sehemu mbalimbali za viungo vya mwili.

Aidha, Kamanda Mutafungwa amewapongeza madaktari, wauguzi, na wafanyakazi wote wa hospitali hiyo kwa upendo mkubwa walionao kwa wagonjwa. Pia, ameeleza kuwa wameshuhudia wagonjwa wenyewe wakieleza namna wanavyopata huduma nzuri.
"Wengine hawana uwezo wa kifedha wa kutibiwa, lakini hospitali imekuwa na utaratibu mzuri wa kuwasaidia ili wasipate shida na waendelee na matibabu." aliongeza Kamanda Mutafungwa
Katika hatua nyingine, Kamanda Mutafungwa ameonyesha masikitiko yake kwa namna ajali za barabarani zinavyopunguza nguvu kazi ya Taifa, kwani vijana wengi aliowatembelea wodini hapo walipaswa kuwepo kwenye shughuli zao za uzalishaji mali huku akidokeza kuwa Jeshi la Polisi litahakikisha linasimamia sheria za usalama barabarani na kuendelea kutoa elimu ya kujikinga na ajali.

"Hatuna budi kufanya kazi kuhakikisha kwamba tunazuia ajali za barabarani. Hata hivyo, wajibu mkubwa sana unabaki kwa wananchi wenyewe, wananchi wakiamua kuchukua tahadhari kubwa, ajali hizi zitaweza kupungua." alisema kamanda Mutafungwa
Kwa upande wake, Dkt. Samson Kichiba, ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji ambaye amepokea msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa ushirikiano wao na hospitali hiyo, pamoja na kitendo chao cha kuona umuhimu wa kufanya matendo ya huruma kwa wagonjwa wanaopatiwa matibabu hospitalini hapo.
"Maafande hawa wa mkoa mzima wamechangishana na kufanikisha kuleta misaada mbalimbali kwa wagonjwa wetu ambao wamelazwa wodini huku wakipata huduma kwenye hospitali yetu."

Dkt. Kichiba ameiasa jamii kuona umuhimu wa kutembelea wagonjwa na watu wengine wenye mahitaji kwa kuwafanyia matendo ya huruma, kama lilivyofanya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza.
Baadhi ya wagonjwa, hususani vijana waliolazwa hospitalini hapo kutokana na ajali mbalimbali zinazosababishwa na vyombo vya moto, wameeleza kufarijika sana na msaada huo, hasa baada ya kupatiwa magongo yatakayowasaidia katika hatua za matibabu na kurejea katika shughuli zao za kila siku.
"Tunashukuru sana, kwa sababu kuna wengine walikuwa hawana magongo lakini leo Jeshi la Polisi limetusaidia na kutuletea kila kitu, kwa hiyo tunashukuru," amesema Elias Silvester
Pia, wameliomba Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza lizidi kuwadhibiti madereva wanaokiuka sheria za barabarani na kusababisha ajali zisizo za lazima.
Discussion
Reader comments
0 contributions