Na Daniel Gahu - Katavi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limeadhimisha miaka 20 ya utekelezaji wa mpango wa Polisi Jamii, huku wananchi wakieleza kuwa uwepo wa kitengo hicho umekuwa chachu ya kupunguza matukio ya uhalifu na kuimarisha usalama katika maeneo yao.
Wananchi waliozungumza katika maadhimisho hayo wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuanzisha na kuimarisha mfumo wa Polisi Jamii, wakisema umesaidia kujenga uhusiano wa karibu kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama.

Wamesema kupitia Polisi Jamii wamepata elimu zaidi kuhusu masuala ya usalama, hatua inayowawezesha kutambua viashiria vya uhalifu, kutoa taarifa kwa wakati na kushiriki moja kwa moja katika kulinda amani na usalama wa maeneo wanayoishi.
“Tunashukuru Jeshi la Polisi kwa kuja na Polisi Jamii kwa sababu imetusaidia sana. Wananchi sasa tunaelewa umuhimu wa kutoa taarifa na kushirikiana na polisi, jambo ambalo limechangia kupunguza matukio ya uhalifu katika jamii zetu,” amesema mmoja wa wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani, amesema mpango wa Polisi Jamii umeendelea kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi katika kukabiliana na uhalifu.
Amesema ushirikiano huo umesaidia katika kupata taarifa muhimu kutoka kwa wananchi, kubaini wahalifu na kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya uhalifu, huku akisisitiza kuwa usalama wa jamii ni jukumu linalohitaji ushirikiano wa kila mmoja.

Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Katavi, John Mwaipungu, amesema kitengo hicho kimekuwa kikitoa elimu ya ulinzi shirikishi katika jamii na katika ngazi za kata, kwa lengo la kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu wajibu wao katika kulinda usalama.
Mwaipungu amesema elimu hiyo imekuwa muhimu katika kuwajengea wananchi uwezo wa kushirikiana na Jeshi la Polisi, kutoa taarifa za matukio ya uhalifu na ukatili, pamoja na kushiriki katika kuzuia uhalifu kabla haujatokea.

Katika maadhimisho hayo, wananchi wameendelea kusisitiza umuhimu wa kuimarisha zaidi Polisi Jamii, wakieleza kuwa ukaribu kati ya polisi na wananchi umeongeza uaminifu na kurahisisha utoaji wa taarifa zinazohusu usalama.
Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu na vitendo vya ukatili kwa wakati, likieleza kuwa ushirikiano huo ni msingi muhimu wa kuendelea kuimarisha usalama, amani na utulivu katika jamii ya Katavi.

Discussion
Reader comments
0 contributions