Na Ibrahim Rojala - Geita.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia na linaendelea kumhoji mtu mmoja aitwaye Peter Willium (28), Mhangaza, mkazi wa Itale, Wilaya ya Chato, kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi (ambaye jina na anwani yake imehifadhiwa kwa sababu za kisheria).
Tukio hilo limetokea Mei 31, 2026, majira ya saa 12:00 jioni, katika pori la Ichwankima lililopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Burigi, Chato ambapo inadaiwa kuwa, mtuhumiwa alimkamata mwathirika na kumvutia vichakani ndani ya hifadhi hiyo, kabla ya kutekeleza kitendo hicho cha kikatili.
Hata hivyo, mtuhumiwa alipotenda unyama huo, aliendelea kumzuia mwathirika huku akiwapigia simu ndugu wa mwathirika na kuwadai watume pesa ili amwachie huru, akitishia kumdhuru iwapo hawatatii matakwa hayo.

Kufuatia taarifa hizo, Jeshi la Polisi liliweka mtego uliowezesha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na chunguzi wa tukio hilo unakamilishwa sambamba na taratibu zote za kisheria ili mtuhumiwa afikishwe mahakamani.
Jeshi la Polisi linawapongeza na linawasihi wananchi kuendelea kufichua vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanafunzi, pamoja na kulinda haki, usalama na ustawi wa makundi hayo. Aidha, Jeshi la Polisi linasisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya uhalifu.
Discussion
Reader comments
0 contributions