Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora limefanikiwa kuwakamata watu 128 katika operesheni maalum, misako na doria za magari, miguu pamoja na mbwa, zilizofanyika kwa muda wa siku 50 kuanzia Julai 1, 2026.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Tabora ACP Twaha Lulengelule amesema miongoni mwa waliokamatwa ni watu 16 wanaodaiwa kujihusisha na dawa za kulevya. Watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na jumla ya kilogramu 512 za dawa za kulevya aina ya bangi pamoja na kete 1,200.

Operesheni hiyo pia imehusisha ukamataji wa watu wanaodaiwa kujihusisha na makosa mbalimbali ya jinai, ikiwemo uzalishaji na usambazaji wa pombe haramu. Polisi walifanikiwa kukamata jumla ya lita 273 za pombe haramu aina ya Moshi.
Aidha, katika misako hiyo, Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata nyara za serikali pamoja na kuwakamata watu wanaodaiwa kuhusika na matukio mbalimbali ya uhalifu, ikiwemo makosa ya mauaji.

Aidha Kamanda Lulengelule ameeleza kuwa baadhi ya watuhumiwa waliofikishwa mahakamani wamehukumiwa kifungo cha jela, huku wengine wakipewa adhabu za vifungo vya nje, hatua inayolenga kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake na kuimarisha usalama wa wananchi pamoja na mali zao.
Discussion
Reader comments
0 contributions